Jamaica. Nguli  wa muziki wa Reggae kutoka Jamaica,  Jimmy Cliff, afariki dunia jana akiwa na umri wa miaka 81.

Taarifa ya kifo cha mwanamuziki huyo maarufu wa reggae aliyesaidia kubadilisha muziki wa Jamaica wenye midundo ya kipekee kuwa utambulisho wa kitamaduni duniani, ilithibitishwa na mkewe jana Jumatatu.

“Kwa huzuni kubwa ninawajulisha kwamba mume wangu, Jimmy Cliff, amevuka kwenda upande wa pili kutokana na mshtuko wa kifafa uliotokana na nimonia,” aliandika mkewe, Latifa Chambers, kwenye akaunti yake rasmi ya Instagram.

“Ninawashukuru familia, marafiki, wasanii wenzake na wafanyakazi wenzake ambao wamekuwa sehemu ya safari yake. Kwa mashabiki wake wote duniani, fahamuni kwamba sapoti yenu ilikuwa nguvu yake katika maisha yake ya muziki.”

Kwa zaidi ya miaka arobaini, Cliff aliandika na kuimba nyimbo zilizochanganya reggae na hisia zake za muziki wa folk, soul, ska na rock na kugusa masuala kama siasa, umasikini, ukosefu wa haki na upinzani wa vita.

Cliff, aliyekuwa mpiga ala mbalimbali na mwimbaji wa vibao kama “You Can Get It If You Really Want” na “The Harder They Come,” anachukuliwa kuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa zaidi katika reggae baada ya marehemu Bob Marley, ambaye alishirikiana naye katika hatua za awali za muziki wa Marley.

Cliff alipata umaarufu mkubwa mapema kupitia filamu iliyofanikiwa sana ya mwaka 1972 “The Harder They Come,” ambayo ilimshirikisha kama mwigizaji mkuu na ilitokana kwa kiasi kikubwa na maisha yake ya kukua katika umasikini na kumtambulisha yeye pamoja na muziki wa reggae kwa hadhira ya kimataifa.

Waziri Mkuu wa Jamaica, Andrew Holness, alisema taifa hilo linapaswa kuenzi Cliff, “jitu la kweli la utamaduni ambaye muziki wake uliubeba moyo wa taifa letu na kuufikisha duniani.”

“Muziki wake uliwatia watu moyo wakati wa magumu, ukaivutia vizazi vingi, na ukaisaidia Jamaica kupata heshima ya kitamaduni duniani,” Holness aliongeza.

“Pumzika salama, Jimmy Cliff. Urithi wako unaendelea kuishi katika kila kona ya kisiwa chetu na katika mioyo ya watu wa Jamaica.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *