
London, England. Mambo yanazidi kunoga England. Hadi sasa Arsenal ndio inaonekana kupewa nafasi kubwa ya kushinda taji la ligi hiyo kutokana na mwendelezo wa matokeo mazuri ambayo imekuwa ikiyapata tangu kuanza kwa msimu huu.
Arsenal iliendelea kujikita kileleni wikiendi iliyopita baada ya kuichakaza Tottenham Hotspur kwa mabao 4-1 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Emirates.
Hat-trick ya Eberechi Eze na bao moja kutoka kwa Leandro Trossard yalitosha kukipaisha kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta kileleni mwa msimamo kwa tofauti ya alama sita.
Ilikuwa pia wikiendi nzuri kwa Chelsea, waliopanda hadi nafasi ya pili baada ya kuifunga, Burnley.
Lakini wakati mahasimu hao wawili wa London wakipata ushindi mnono, mambo hayakuwa mazuri kwa Manchester City, ambayo ilijikuta ikivutwa shati baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Newcastle United kwenye Uwanja wa St James’ Park.
Man City imesalia katika nafasi ya tatu lakini sasa iko nyuma kwa pointi saba dhidi ya Arsenal, lakini vita kati ya timu hizi tatu bado inaendelea.
Kumekuwa na imani kubwa kwamba katika mechi tano zijazo, huenda ikatolewa taswira halisi ya timu ambayo inaweza kuibuka na ubingwa wa EPL msimu huu kwa kuzingatia zile timu ambazo zinaminyana katika nafasi tatu za juu kwa sasa.
Kinara wa ligi Arsenal baada ya kuisambaratisha Spurs, katika mechi tano zijazo ina mtihani mwingine mgumu wikiendi ijayo itakaposafiri kwenda Stamford Bridge kuvaana na Chelsea iliyopo nafasi ya pili. Ikiwa itapata ushindi katika mchezo huo, basi njia yao ya kulitwaa taji itazidi kuwa safi kwani itakuwa imejikita kileleni kwa tofauti ya alama tisa.
Baada ya mechi hiyo, siku tatu baadaye, Arsenal itaikaribisha Brentford kwenye dimba la Emirates kisha itakwenda Villa Park kukutana na Aston Villa inayonolewa na aliyewahi kuwa kocha wao, Unai Emery.
Mwanzoni mwa Desemba, itakutana na Wolves iliyopo kwenye wakati mgumu kisha mechi yao ya tano watacheza dhidi ya Everton.
Chelsea ambayo inaonekana kuwa katika kiwango bora kwa sasa katika mechi tano zijazo ya kwanza itakuwa ni dhidi ya Arsenal. Mechi hii kwa Chelsea itakuwa na maana kubwa sana ikiwa itashinda kwani itazidi kuisogelea Arsenal na tofauti itakuwa alama tatu tu.
Baada ya mechi hiyo, Chelsea itaelekeza macho katika mechi ya ugenini dhidi ya Leeds United kwenye Uwanja wa Elland Road ambao utakuwa wa kwanza kwa Desemba. Wiki inayofuata itacheza mechi nyingine ugenini dhidi ya Bournemouth.
Mechi itakayofuatia itakuwa ni dhidi ya Everton Desemba, 13, kwenye dimba la Stamford Bridge.
Mechi yao ya tano itakuwa ni dhidi ya Newcastle United kwenye dimba la St James’ Park.
Licha ya kuwa nyuma kwa pointi saba dhidi ya kinara Arsenal, Manchester City inaonekana kuwa inaweza kupindua meza katika mechi zao tano zijazo kwa kuangalia ratiba na rekodi zao.
Wikiendi ijayo, itaikaribisha Leeds United yenye hali mbaya kwenye uwanja wao wa Etihad.
Baada ya hapo, City itasafiri kwenda Craven Cottage kukutana na Fulham kabla ya kukaribisha Sunderland nyumbani na mechi mbili za mwisho itacheza dhidi ya timu za London ambazo ni Crystal Palace nyumbani na West Ham United ugenini.