Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNCTAD limesema Jumanne kuwa ujenzi mpya wa Ukanda wa Gaza utagharimu zaidi ya dola bilioni 70 za Kimarekani na huenda ukachukua miongo kadhaa. Shirika hilo limetoa wito kwa jumuia ya kimataifa kuingilia kati kwa ”haraka” na kwa ”umuhimu mkubwa”

Katika ripoti yake iliyoitoa Jumanne, UNCTAD umeonya kuwa vita na vikwazo vimesababisha “kuporomoka kusikotarajiwa kwa uchumi wa Palestina”. Kulingana na ripoti hiyo, operesheni za kijeshi zimedhoofisha kwa kiasi kikubwa kila nguzo ya maisha, kuanzia chakula hadi makaazi hadi huduma ya afya, na kuitumbukiza Gaza katika shimo lililotengenezwa na binadamu. Uharibifu unaoendelea na wa kimfumo unatia shaka kubwa juu ya uwezo wa Gaza kujijenga upya kama nafasi na jamii ambayo watu wanaweza kuishi.

Uharibifu umesababisha migogoro mikubwa Gaza

Aidha, UNCTAD imetoa wito wa kuwepo ”mpango kamili wa uokoaji” ukichanganya na misaada ya kimataifa iliyoratibiwa, urejeshaji wa miamala ya kifedha na hatua za kupunguza vikwazo kwenye biashara, mchakato na uwekezaji. Kiwango cha uharibifu kilichotokea Gaza kimefichua migogoro mikubwa ya kiuchumi, kiutu, kimazingira na kijamii, na hivyo kuisukuma katika kukosekana maendeleo hadi kutokea kwa uharibifu mkubwa.

Wakati huo huo, makundi ya wanamgambo ya Kipalestina ya Hamas na Islamic Jihad wamesema watakabidhi mabaki ya mateka mmoja wa Gaza baadae Jumanne, chini ya masharti ya kusitisha mapigano na Israel yaliyosimamiwa na Marekani. Vikosi vya al-Quds Brigades na Ezzedine al-Qassam vitaukabidhi mwili huo wa mateka wa Israel aliyepatikana katikati mwa Ukanda wa Gaza majira ya saa kumi kamili jioni kwa saa za Gaza.

Jeshi la Israel limelishambulia gari Gaza, licha ya kuwepo makubaliano ya kusitisha mapigano
Shambulizi la jeshi la Israel katika Ukanda wa GazaPicha: IMAGO/Anadolu Agency

Mapema Jumanne, Israel ilisema kuwa kuchelewa kukabidhiwa kwa miili ya mateka ambaye Islamic Jihad ilisema iliupata jana Jumatatu, ulikuwa ni ”kukiuka” makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano. Wanamgambo hao bado wanashikilia mabaki ya mateka watatu katika Ukanda wa Gaza.

Ama kwa upande mwingine, jeshi la Israel limesema vikosi vyake vimemuua kwa kumpiga risasi mwanaume wa Kipalestina ambaye wamesema alimuua raia wa Israel. Wizara ya afya ya Palestina imethibitisha kifo cha Mpalestina huyo aliyeuawa karibu na mji wa Jenin, katika Ukingo wa Magharibi. Ghazi Ali Mrahin, jirani na yalipotokea mauaji hayo, amesema waliamriwa kutoka kwenye makaazi yao.

Mashambulizi ya Jenin na Nablus

”Tulikaa hapo kwa saa mbili na mikono yetu ikiwa hewani, na kisha aliuawa. Hatujui hasa kilichotokea, walifyatua tu kombora na kushambulia nyumba iliyo karibu na yetu. Hatujui kama majirani zetu walikuwa ndani,” alifafanua Mrahin.

Katika taarifa ya pamoja, jeshi na Idara ya Usalama wa Ndani ya Shin Bet, vimesema vikosi karibu na Jenin vilimuondoa gaidi ambaye alifanya shambulizi la kigaidi dhidi ya Gideon Perry. Jeshi limesema limewakamata washirika wake watano wakati wa operasheni ya kijeshi iliyofanyika usiku wa kuamkia Jumanne.

Jumatatu, jeshi lilianzisha mashambulizi kwenye mji wa Nablus na kumuua Mpalestina mmoja ambaye aliwaua wanajeshi wawili katika shambulizi lililotokea kwenye mji huo mwezi Mei mwaka 2024.

(AFP, DPA, Reuters)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *