
Rais Vladimir Putin wa Russia amesema kuwa, vipengele vya rasimu ya amani vilivyojadiliwa hivi karibuni na Marekani na Ukraine vinaweza kutumika kama msingi wa makubaliano ya siku zijazo ya kukomesha vita nchini Ukraine.
Akizungumza na waandishi wa habari huko Bishkek, Putin amesema kuwa, Washington na Kyiv zimeligawanya pendekezo la nukta 28 katika vipengele vinne wakati wa mazungumzo huko Geneva – na kwamba Moscow ilikuwa imearifiwa kuhusu mchakato huo. Kwa nujibu wa Putin, Russia “kwa ujumla inakubali” kwamba vipengee hivyo vinaweza kuwa mwongozo wa mazungumzo ya siku zijazo.
Rais Putin amesisitiza kwamba hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa hadi hivi sasa kuhusu rasimu hiyo, kwani hiyo iliyopo ni orodha tu ya masuala ambayo pande zote zimekuwa zikiyachunguza. Amebainisha kuwa mada hizo zilijadiliwa huko nyuma na wapatanishi kabla ya ziara yake nchini Marekani, na baadaye zilitumwa Moscow kwa ajili ya kujadiliwa zaidi.
Rais huyo wa Russia amesisitizia pia umuhimu wa kutumika lugha makini ya kidiplomasia akisema kwamba kila neno katika makubaliano hayo litakuwa ni muhimu.
Ameongeza kwamba ikiwa nchi za Magharibi zinahitaji uhakikisho wa maandishi kutoka kwa Russia, Moscow itakuwa tayari kutoa uhakikisho huo.
Rais Putin pia ameonya kwa kusema kwamba ni mapema mno hivi sasa kuzungumzia natija ya mchakato huo au kuhusu makubaliano kamili.
Wakati huo huo taarifa zinasema kuwa, ujumbe wa Marekani unatarajiwa kuwasili Moscow wiki ijayo kwa majadiliano zaidi, ikiwa ni ishara kwamba juhudi zinaendelea za kuchunguza njia inayoweza kumaliza vita vya Ukraine na kufikia amani ya kudumu.