
Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO limetoa mwongozo wake wa kwanza kuhusu matumizi ya kundi jipya la dawa za kupunguza uzito, hatua inayowakilisha mabadiliko makubwa katika sera za afya duniani wakati viwango vya unene wa kupitiliza au utipwatupwa vikizidi kuongezeka.
Mwongozo huo unalenga tiba za dawa aina ya GLP-1 ambazo ni dawa kama vile liraglutide, semaglutide na tirzepatide na linatoa mapendekezo ya masharti kuhusu jinsi zinavyoweza kutumika kwa usalama kama sehemu ya matibabu ya muda mrefu.
Kwa mujibu wa takwimu za WHO zaidi ya watu bilioni moja duniani wanaishi na unene uliokithiri au utipwatipwa, hali iliyohusishwa na vifo milioni 3.7 mwaka 2024.
Bila kuchukua hatua madhubuti, WHO inaonya kuwa idadi ya watu watakaoathirika inaweza kuongezeka mara mbili kufikia 2030, na hivyo kuongeza mzigo mkubwa kwa mifumo ya afya na kusababisha hasara za kiuchumi duniani zinazokadiriwa kufikia dola trilioni 3 kwa mwaka.
Kama mamlaka kuu ya afya ya umma duniani, taarifa ya WHO inatarajiwa kuathiri sera za kitaifa, bima za afya na mazoea ya kitabibu, hasa wakati mahitaji ya tiba bora za kupunguza uzito yakiongezeka kwa kasi.
WHO inasisitiza kuwa unene kupita kiasi si matokeo ya uchaguzi wa mtindo wa maisha pekee, bali ni hali tata na sugu inayohusisha vinasaba, mazingira, biolojia na hali za kijamii.
Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO amesema utipwatipwa “Ni kichocheo kikuu cha magonjwa ya moyo, kisukari aina ya pili na aina fulani za saratani, na pia huongeza hatari kwa magonjwa ya kuambukiza. Kwa watu wengi, kupunguza uzito na kuudumisha ni jambo gumu bila msaada wa kitabibu.”
WHO inasisitiza kuwa dawa za kupunguza uzito zinapaswa kutumika sambamba na msaada mwingine.
Matibabu yenye ufanisi zaidi yanachanganya dawa na ulaji bora, kuongeza shughuli za mwili, na ushauri wa muda mrefu kutoka kwa wahudumu wa afya.