
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa sehemu muhimu za maelewano yanyolenga kumaliza vita vilivyolazimishwa zinakaribia kukamilika, pamoja na kuwepo misimamo kinzani ya Washington na vitendo vya mara kwa mara vya uchokozi wa kijeshi vinavyolenga kuvuruga mchakato wa kidiplomasia.
Katika mahojiano jioni ya Alhamisi, Esmaeil Baghaei amekanusha uvumi wa vyombo vya habari kuhusu kufikiwa kwa makubaliano na akasisitiza tena msimamo thabiti na wa kimsingi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Baghaei amesema, “Kwa upande wa maandishi, rasimu ya makubaliano imekaribia kukamilika katika sehemu zake kuu. Tatizo ni kwamba misimamo kinzani ya Marekani imekuwa mara kwa mara chanzo cha misukosuko na kuvuruga mchakato huu.”
Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu iliingia katika mchakato wa kidiplomasia kwa nia njema na kwa uwajibikaji kamili, huku maafisa wa Marekani wakibadili mara kwa mara misimamo yao, wakitoa madai mapya yasiyo ya uhalisia, na hata kufanya mashambulizi ya kijeshi wakati mazungumzo yakiendelea.
Baghaei amebainisha kuwa tangu tangazo la usitishaji mapigano mwezi Aprili, Marekani na utawala wa Israel wamekiuka mara kadhaa makubaliano hayo ya kusitisha vita.
Katika mashambulizi ya hivi karibuni, vikosi vya Marekani vililenga miundombinu ya kusini mwa Iran na kushambulia mabwawa mawili ya maji katika eneo la Sirik, kitendo ambacho ni jinai ya kivita.
Amesisitiza wazi kwamba Iran imeonyesha, katika diplomasia na pia katika uwanja wa mapambano, kwamba haitakubali kamwe masharti na matakwa ya upande wa pili.
Baghaei amesisitiza kuwa: “Iran imeonyesha kwa vitendo kwamba mistari yake myekundu ni maslahi na ustawi wa taifa la Iran, na hakutakuwa na maafikiano yoyote yanayokiuka hilo.”
Ameongeza kuwa: “Lau Jamhuri ya Kiislamu ingekuwa na nia ya kurudi nyuma kutoka katika misimamo yake ya kimsingi chini ya shinikizo na vitisho, ingefanya hivyo mwaka mmoja na nusu uliopita. Tumeonyesha kwamba tunasimama imara.”
Mlango Bahari wa Hormuz wafungwa kutokana na uchokozi wa Marekani
Akizungumzia hali katika Mlango Bahari wa Hormuz, Baghaei amesema kuwa licha ya hatua za kuwajibika za Iran za kuhakikisha usalama wa njia za baharini, Marekani imefanya njia hiyo muhimu ya kimkakati kuwa hatarishi kupitia mashambulizi yake ya kijeshi.
Kufuatia mashambulizi ya Marekani dhidi ya vituo vya Iran kusini mwa nchi pamoja na mashambulizi mabaya dhidi ya meli za kibiashara, ikiwemo meli tatu za India ambapo mabaharia wa India wamefariki, Iran imetangaza kufungwa kwa Mlango Bahari huo kwa meli zote.
Baghaei amesema sababu pekee ya hali hii ni vitendo visivyo halali na vya uchokozi vya Marekani.
Uamuzi uko mikononi mwa mamlaka ya Iran
Aidha amesema: “Mchakato wa kufanya maamuzi katika nchi yetu uko wazi kabisa. Mamlaka husika lazima zipitie kila undani wa maandishi ya makubaliano. Pindi tu tutakapofikia hitimisho la mwisho linalolinda maslahi ya taifa la Iran, jambo hilo litatangazwa rasmi.”
Baghaei ameongeza kuwa wapatanishi kutoka Pakistan na Qatar wanaendelea na juhudi zao, ingawa njia ya kidiplomasia kwa kawaida imeathiriwa na vitendo vya uchokozi vya Marekani.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje aamehitimisha kwa kusisitiza tena msimamo thabiti wa Iran kwamba katika mazungumzo au makubaliano yoyote, Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuzingatia kikamilifu kulinda na kuendeleza maslahi na haki za wananchi wa Iran.