
Mamlaka ya mpito ya Haiti siku ya Jumanne Desemba 2, imetangaza kalenda ya uchaguzi uliokuwa unasubiriwa kwa muda mrefu , ikibainisha kwamba nchi hiyo, inayokabiliwa na mgogoro mkubwa, inapanga kufanya uchaguzi wake wa kwanza katika kipindi cha karibu muongo mmoja mnamo mwezi wa Agosti. Hii ni hatua muhimu kuelekea kurejesha demokrasia, hata kama maafisa wanaonya kwamba vurugu za magenge zilizoenea bado zinatishia kuvuruga mchakato huo.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Haiti, ikiwa imedhoofika na magenge, ilichukua hatua kubwa siku ya Jumanne ikitangaza kufanyika kwa uchaguzi wake wa kwanza katika kipindi cha karibu muongo mmoja, baada ya mamlaka ya mpito kutangaza kwamba nchi hiyo ingepiga kura msimu ujao wa kiangazi.
Duru ya kwanza ya uchaguzi mkuu itafanyika mwezi Agosti 2026, lakini kurejesha usalama kote nchini ni muhimu kwa ajili ya kufanyika kwa uchaguzi, kulingana na Baraza la Uchaguzi la Muda, chombo kilichotangaza amri hiyo na kinachohusika na kuandaa uchaguzi.
“Kurejesha usalama ni sharti la kufanyika kwa duru ya kwanza” ya uchaguzi wa wabunge na urais, ametangaza Waziri Mkuu Jacques Desrosiers.
Haiti, nchi maskini zaidi barani Amerika, inakabiliwa na migogoro ya kisiasa na usalama kwa muda mrefu. Hali ilikuwa mbaya zaidi tangu mwanzoni mwa mwaka 2024, wakati Waziri Mkuu Ariel Henry alipolazimishwa kujiuzulu na makundi yenye silaha ambayo bado yanadhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu, Port-au-Prince.
Haiti haijafanya uchaguzi tangu mwezi Oktoba 2016. Rais wake wa mwisho aliyechaguliwa, Jovenel Moïse, aliuawa mnamo mwezi Julai 2021.
Baraza la mpito, Baraza la Rais wa Mpito, kwa sasa linaongoza nchi hiyo, lakini mamlaka yake inamalizika mnamo mwezi Februari 2026.
Laurent Saint-Cyr, rais wa Baraza, amekaribisha kupitishwa kwa amri hiyo, akibainisha kwamba uamuzi huu “hatimaye unawapa watu wa Haiti fursa ya kuchagua kwa uhuru na uwajibikaji wale watakaowaongoza.”
“Kwa kuchukua hatua hii muhimu, huku tukiendelea kujitolea kikamilifu kurejesha usalama, tunathibitisha tena kujitolea kwetu kuirudisha Haiti kwenye njia ya uhalali na utulivu wa kidemokrasia,” ameongeza katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Magenge ya wahalifu yamesababisha ukosefu wa utulivu nchini Haiti, yakiendesha mauaji, ubakaji, uporaji, na utekaji nyara kote nchini.
Mwaka wa 2023, Umoja wa Mataifa uliidhinisha ujumbe wa usalama wa kimataifa ili kuwasaidia polisi wa Haiti waliozidiwa nguvu katika kupambana na magenge, lakini kutmwa kwa ujumbe huo usio na vifaa na ufadhili wa kutosha umeweka yake katika hali tatanishi.
Mwishoni mwa mwezi Septemba, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha mabadiliko ya ujumbe huo kuwa kikosi imara zaidi cha kupambana na magenge.
Umoja wa Mataifa uliripoti mnamo mwezi Oktoba kwamba zaidi ya watu 16,000 waliuawa na vurugu hizo nchini Haiti tangu mwanzo wa mwaka 2022.