Hayo ni kwa kwa mujibu wa mshauri wa serikali ya Kremlin Yury Ushakov aliyeviambia vyombo vya habari vya Urusi baada ya kikao kilichodumu takribani saa tano.
Jared Kushner, mkwe wa Trump, pia alihudhuria kikao hicho kilicholenga kujadili mipango ya kumaliza vita vya Urusi dhidi ya Ukraine. Ushakov alisema mazungumzo yalikuwa ya kujenga, yenye maudhui yenye tija. Aliongeza kuwa baada ya mazungumzo hayo, pande hizo zimeonekana kutokuwa mbali na amani, ingawa pia hazijakaribia suluhu ya mgogoro huo.
Hakuna mabadiliko kuhusu madai ya Urusi kwa Ukraine
Mshauri huyo wa Kremlin alisema bado hakuna makubaliano kuhusu madai ya Urusi ya kupewa maeneo ya Ukraine. Putin anasisitiza kuwa Ukraine lazima ikubali kuachia eneo la mashariki la Donbass ili kufikia amani, ikiwemo maeneo ambayo majeshi ya Urusi yameshindwa kuyateka kwa zaidi ya miaka mitatu na nusu ya vita. Jambo ambalo linakataliwa vikali na serikali ya Kiev.
Mpango wa amani wa Marekani wenye vipengele 28 ulitangazwa mwishoni mwa Novemba. Hata hivyo, umepitia mabadiliko kadhaa katika siku za hivi karibuni kwa sababu mapendekezo mengi ya awali hayakukubalika kwa Ukraine na Umoja wa Ulaya. Hivi karibuni, Marekani na Ukraine zimekuwa zikishirikiana kuuboresha mpango huo.
Zelenskiy: Bado kuna nafasi ya kuboresha makubaliano ya amani
Kwa zingatio hilo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amenukuliwa akisema kwamba wajumbe wa Marekani na Ukraine wame “wataboresha” makubaliano ya msingi ya amani yaliyotengenezwa mjini Geneva wakati wa mazungumzo yao ya hivi karibuni huko Florida.
Kupitia chapisho lake kwenye mtandano wa X, amesema Ukraine inataka washirika wake wa kigeni zaidi washiriki katika mchakato huo. Pia aliiitupia lawama Urusi kuwa imeanzisha “kampeni za upotoshaji” kabla ya mkutano kati ya maafisa wa Marekani na Urusi.
Zelensky ambae yupo ziarani Ireland, amesema taifa hilo ni moja kati ya machache barani humo kuelewa gharama ya uhuru huku akilisifu taifa hilo kwa msaada wake. Katika ziara yake hiyo ya kwanza Zelensky na Waziri Mkuu wa Ireland Micheal Martin wote walilinganisha mapambano ya Ukraine ya kutetea uhuru wake na vita vya karne nyingi vya Ireland vya kupigania uhuru.