Akizungumza kutoka Makao Makuu ya Ofisi ya Haki za Binadamu OHCHR mjini Geneva, Uswisi, Türk amesisitiza umuhimu wa mazingira huru ya kisiasa, na ameitaka serikali kuhakikisha inalinda na kuheshimu haki za binadamu kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Ukamatwaji wa wafuasi wa upinzani waongezeka

Kwa mujibu wa taarifa za kuaminika, takribani watu 550, wakiwemo wanachama na wafuasi wa chama cha upinzani cha National Unity Platform (NUP), wamekamatwa na kuzuiliwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Aidha, zaidi ya watu 300 wamekamatwa tangu kampeni zilipoanza mwezi Septemba, na wengi wao bado wako rumande wakikabiliwa na mashtaka mbalimbali kama vile kusababisha usumbufu, kukaidi maagizo halali na kuchochea vurugu.

Matumizi ya nguvu kupita kiasi yavuruga kampeni

Katika kipindi chote cha kampeni, Kamishina Mkuu anasema vikosi vya usalama vimeripotiwa kupelekwa kwa wingi katika maeneo ambayo NUP inapanga kufanya mikutano. 

Kwa mfano, wiki iliyopita katika mji wa Iganga uliopo kaskazini mashariki mwa Uganda askari waliripotiwa kutumia risasi za moto na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine watatu.

Zaidi ya hayo, mabomu ya machozi, virungu, mijeledi, magari ya maji ya kuwasha na kemikali zilitumiwa kuwatawanya wafuasi wa upinzani, na kujeruhi watu wengi.

Itasikitisha sana kuona kampeni zikichafuliwa tena na ukamataji holela, vizuizi visivyo na msingi na matumizi ya nguvu kupita kiasi,” amesema Türk akiwa mjini Geneva.

Utekaji, mateso na vizuizi visivyo rasmi yaongezeka

Katika kipindi cha mwaka uliopita kwa mujibu wa OHCHR kumekuwa na ongezeko la taarifa za watu kukamatwa kiholela, kuteswa na hata kupotezwa kwa nguvu.

Vikosi vya usalama vimetuhumiwa kutumia magari yasiyotambulika, yanayojulikana kama “drones”, kuwahamisha watu hadi maeneo yasiyo rasmi ya kizuizi, maarufu kama “safe houses”, ambako wanashikiliwa bila mawasiliano.

Kinyume na sheria za kimataifa, mashirika ya haki za binadamu yanasema watuhumiwa wanapaswa kuzuiliwa tu katika maeneo yanayotambuliwa rasmi ili kuzuia mateso.

Katika tukio la mwezi Mei, Mkuu wa Majeshi aliandika kwenye mtandao wa X akieleza kwamba anamshikilia mlinzi wa kiongozi wa NUP “kwenye basement” yake. 

Baada ya malalamiko ya umma, mlinzi huyo alipelekwa mahakamani akiwa anatetemeka na kuonesha dalili za mateso, bila hatua yoyote ya uchunguzi kuchukuliwa.

Vilevile, wanaharakati wawili kutoka Kenya waliokamatwa baada ya kuhudhuria mkutano wa upinzani mwezi Oktoba,  walizuiliwa kwa zaidi ya mwezi mmoja katika maeneo ya siri ambayo Rais aliwahi kuyaita “friji”, kabla ya kukabidhiwa kwa mamlaka za Kenya.

Aidha, makumi ya wafuasi wa upinzani bado wanashikiliwa tangu uchaguzi mkuu uliopita zaidi ya miaka minne iliyopita.

Uchunguzi huru na uhuru wa vyombo vya habari 

Nazitaka mamlaka za Uganda kufanya uchunguzi kamili, huru na usio na upendeleo kuhusu madai haya yote ya kutoweshwa kwa nguvu, ukamataji holela na mateso,” amesema Türk akihutubia kutoka Geneva. “Watu wote waliokamatwa kiholela waachiwe mara moja.”

Kwa upande wa uhuru wa vyombo vya habari, Türk ameendelea kuonesha wasiwasi wake kufuatia matukio ya kudhibiti vyombo vya habari katika miezi ya hivi karibuni. Mwezi Oktoba, waandishi wa NTV Uganda na gazeti la Daily Monitor walinyang’anywa vibali vyao vya kuripoti bungeni kutokana na taarifa zilizoonekana kukosoa watawala.

Katika uchaguzi mdogo wa mwezi Machi, eneo la Kawempe North lililopo kaskazini magharibi mwa Jiji la Kampala waandishi 32 waliripotiwa kushambuliwa, kupokonywa vifaa au kuvunjwa kamera zao na maafisa wa usalama.

Türk amehitimisha kwa kusisitiza serikali ya Uganda kukomesha matumizi ya nguvu dhidi ya vyombo vya habari na wapinzani, na kuhakikisha inatimiza wajibu wake chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *