Rais wa Urusi, Vladimir Putin, anaanza ziara ya siku mbili nchini India katika juhudi za kuimarisha ushirikiano, hususan katika sekta ya ulinzi. Ziara hii inafanyika wakati India inakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka Marekani ikiitaka New Delhi iachane na ununuzi wa mafuta kutoka Urusi.

Ziara hiyo ni ya kwanza ya kiongozi huyo nchini humo tangu Moscow ilipoivamia Ukraine. Miongoni mwa ujumbe alioambatana nao Putin ni Waziri wa Ulinzi Andrei Belousov.

Rais huyo wa Urusi, anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu Narendra Modi watakaposhiriki pamoja dhifa maalumu ya faragha baadaye jioni. Dhifa hiyo itafuatiwa na mkutano pamoja na mazungumzo na wafanya biashara yatakayofanyika Ijumaa.

Msemaji wa Ikulu ya Urusi, Kremlin, Dmitry Peskov, awali alieleza kuwa moja ya ajenda muhimu zitakazozungumziwa na viongozi hao wawili katika kuimarisha ushirikiano wa kiusalama ni pamoja na suala la Moscow kuipatia India mifumo ya ulinzi wa anga ya kisasa inayofahamika kama S-400.

Ripoti za vyombo vya habari vya India zinasema pia kuwa huenda Urusi ikapendekeza kushirikiana na New Delhi kwenye utengenezaji wa ndege za kivita za Urusi chapa Su-57. India ni moja kati ya mataifa yanayonunua zaidi silaha kutoka nje na Urusi ndiyo msambazaji wake mkubwa.

Kando ya ushirikiano wa kiusalama, mahusiano ya kibiashara yanatarajiwa kuwemo kwenye ajenda ya mazungumzo mjini Delhi huku wizara ya mambo ya nje ikiuelezea ushirikiano kati ya nchi yake na Urusi kuwa ndiyo uhusiano thabiti zaidi katika nyakakati hizi. 

Shinikizo la Marekani kwa India kususia mafuta ya Urusi

Ziara ya Vladimir Putin inafanyika baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuziwekea ushuru wa asilimia 50 bidhaa nyingi za India mnamo mwezi Agosti. Hatua hiyo ilichukuliwa kama adhabu ya India kwakununua mafuta ya Urusi.

Putin anaanza ziara yake nchini India 04.12.2025
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Alexander Kazakov/Sputnik/REUTERS

Ieleweke kuwa, nchi hiyo imeendelea kuwa mteja wa mafuta ya Urusi inayoyapata kwa bei nafuu licha ya maonyo kadhaa yaliyotolewa na Marekani inayodai kuwa biashara hiyo ndiyo inayoipa Urusi mapato ya kuendeleza vita Ukraine.

India yenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani imekuwa mnunuaji mkubwa wa mafuta hayo ya Urusi kwa bei nafuu na kuokoa mabilioni ya dola. Hilo limeipa Moscow soko kubwa inalolihitaji baada ya wateja wake wakubwa wa Ulaya kusitisha kununua mafuta ya Urusi kwa sababu ya vita.

Duru za habari zinasema India inahofia kuwa makubaliano mapya ya nishati na usalama na Urusi yanaweza kumkasirisha Trump na matokeo yake yanaweza kuwa mabaya katika mazungumzo ya kibiashara yanayoendelea na Washington. Hata hivyo msemaji wa Kremlin amebainisha kuwa Urusi kwa upande wake haijali lolote kuhusu ushuru wa Marekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *