
Onyo hili, lililotolewaleo nchini Msumbiji, linakuja wakati ongezeko hilo la wakimbizi wa ndani linaendelea kulemeza huduma za msingi na riziki za wananchi.
Kwa kuzingatia hali hiyo, Bi. Pope ametoa wito wa utekelezaji wa pamoja wa suluhu za kudumu ili kusaidia jamii kurejesha uthabiti na kuimarisha maisha yao kwa muda mrefu.
Katika ziara ya kikazi ya siku tatu nchini humo, Bi.Pope amesisitiza jinsi ukosefu wa usalama kaskazini mwa nchi pamoja na misururu ya majanga ya tabianchi, yakijumuisha mafuriko, ukame na vimbunga, vinavyoendelea kusababisha uhamishaji na kudhoofisha upatikanaji wa huduma na riziki.
Uwekezaji endelevu unatakiwa
Bi. Pope ametoa wito wa kuongezwa kwa uwekezaji katika juhudi za urejeshaji zinazoongozwa na jamii ambazo zinaweza kuwasaidia wananchi kujenga upya maisha yao, kurejesha huduma muhimu na kuelekea mnepo wa muda mrefu.
“Athari za miaka ya ukosefu wa usalama na misukosuko ya tabianchi bado zinahisiwa kwa kina nchini Msumbiji. Hata hivyo, maendeleo niliyoyaona wiki hii yanaonesha kuwa jamii, zinapopata msaada, zinaweza kuongoza kujikwamua na kujenga upya hali ya uthabiti. Kwa uwekezaji sahihi, familia zinaweza kusimama tena, kuimarisha mnepo wao, na kuutazama mustakabali kwa kujiamini.” amesema Bi. Pope
Katika mazungumzo na Mheshimiwa Daniel Francisco Chapo, Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, pamoja na maafisa waandamizi wa Serikali, Pope amekiri juhudi za nchi hiyo za kuimarisha mnepo na kupanua fursa za kiuchumi kwa jamii zilizoathiriwa na uhamishaji.
Mazungumzo hayo yamebainishajinsi juhudi za kitaifa na kimataifa zinavyoweza kuimarisha maendeleo ya Msumbiji kuelekea kujikwamua nakujenga mnepo wa muda mrefu.
Mazungumzo na waathirika
Huko Corrane, katika Mkoa wa Nampula, Bi. Pope amekutana na familia zilizoathirika na za wenyeji wanaofanya kazi pamoja kujijengea maisha upya.
Wamemweleza naye jinsi maboresho ya kivitendo kama makazi imara, kituo cha jamii, huduma bora za maji na usafi wa mazingira, na upatikanaji wa huduma za afya za kuaminika vinavyoboresha usalama na uthabiti katika maisha yao ya kila siku.
Miradi hii, inayoongozwa na jamii kwa ushirikiano na Serikali, Taasisi ya Taifa ya Usimamizi wa Majanga na Kupunguza Hatari (INGD), IOM na washirika wa Umoja wa Mataifa, na inazipa familia ujasiri wa kuanzisha biashara ndogo ndogo, kurejea shuleni na kupanga mustakabali wao.
Katika mikoa iliyoathirika, familia na viongozi wa mitaa wanaendeleza juhudi hizi kwa kurejesha upatikanaji wa makazi, huduma na riziki.
Uzoefu wa Msumbiji katika kukabiliana na ufurushwaji wa watu unaotokana na migogoro na majanga ya tabianchi unaifanya nchi hiyo kuwa kitovu cha mijadala ya kikanda kuhusu mnepo na ufurushwaji wa watu.
Mkakati wa Msumbiji 2024-2028 wazinduliwa
Wakati wa ziara hiyo, Mkuu huyo wa IOM pia amezindua mkakati wa IOM wa nchi ya Msumbiji (2024–2028) na ripoti ya viashiria vya utawala wa uhamiaji, iliyotayarishwa kwa pamoja na serikali.
Mfumo huo unaainisha madhumuni ya pamoja ya kuimarisha utawala wa uhamiaji kwa watu walioko katika harakati. Vyote viwili vinaelekeza mipango ya vitendo ya muda mrefu ili jamii ziweze kupata huduma na fursa wanazohitaji.
Ziara hiyo pia imewaunganisha wadau wa taasisi za fedha za maendeleo ili kuchunguza mbinu mpya za kufadhili uthabiti na riziki endelevu. Majadiliano haya yataarifu mashauriano yajayo ya kikanda nchini Afrika Kusini, yakisaidia kuoanisha vipaumbele vya kitaifa na ajenda pana ya uhamaji na maendeleo katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Ziara ya Bi. Pope imesisitiza tena dhamira ya IOM ya kuunga mkono suluhu zinazoongozwa na serikali na jamii ambazo zinaimarisha uthabiti, kukuza ujumuishaji wa kiuchumi, na kuchangia amani na uthabiti wa kudumu katika eneo hilo. Maendeleo haya yanadhihirisha uongozi wa jamii ambazo zinaunda mustakabali wao kwa msaada wa taasisi za kitaifa na za mitaa zinazofanya kazi kwa pamoja kuandaa mazingira ya kudumu ya kujikwamua.