
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imesema kuwa, imeidhinisha kusamehewa Somalia karibu dola milioni 18 na hivyo kufungua njia ya kufutwa kabisa mikopo yote ya nchi hiyo ambayo inajumuisha ya kipindi cha baina ya mwaka 2024 hadi 2039.
Benki hiyo imesema, imechukua hatua hiyo baada ya ustawi kuanza kuonekana Somalia na nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi, usimamizi mzuri wa fedha za umma, uhamasishaji wa mapato ya ndani na utawala bora.
“Msamaha huu wa deni unafungua mlango wa kuundwa taasisi imara, huduma bora, na matumaini mazuri kwa raia wa Somalia huku athari zikionekana katika maskuli, kliniki, mashamba na masoko kote nchini Somalia,” amesema Mshauri Mkuu wa Uendeshaji wa Benki ya AfDB kwa Somalia, Bubacarr Sankareh katika taarifa yake ya jana Jumatano.
Kwa mujibu wa Benki ya AfDB, Somalia pia imetimiza ahadi zake za kupunguza umaskini kwa kuboresha utoaji wa huduma za msingi na kupanua misingi ya kulinda usalama wa familia zinazoishi kwenye magumu.
Benki hiyo pia imesema kuwa, msamaha huo wa deni umekuja kufuatia kukamilika kwa mafanikio mchakato wa Mpango wa Nchi Maskini Zilizo na Madeni Makubwa, na utapunguza deni la nje la Somalia kwa dola milioni 17.68 za Kimarekani.
Mpango huo, uliozinduliwa mwaka wa 1996 na Benki ya Dunia, unafanya kazi ya kupunguza mzigo wa madeni usioweza kudhibitiwa kwa nchi zinazokidhi vigezo vikali na kujitolea kuendesha sera za kupunguza umaskini, kuleta ustawi wa kiuchumi na kupunguza umaskini.