Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema hasira ya Israel kuhusu hati ya maelewano (MoU) ya makubaliano kati ya Iran na Marekani inaashiria wazi mafanikio na ushindi wa taifa la Iran.

Rais Pezeshkian ametoa kauli hiyo katika hotuba yake kwenye mkutano wa kitaifa jana Jumatatu, siku moja baada ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran (SNSC) kutangaza kwamba limekamilisha hati ya maelewano ya mkataba wa kukomesha vita (MoU) kati ya Tehran na Washington.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kusimamisha vita mara moja na daima katika pande zote, ikiwemo Lebanon, na kukomesha mzingiro wa majini wa Marekani dhidi ya Iran. Hati hiyo itasainiwa rasmi mjini Geneva, Uswisi, tarehe 19 Juni.

“Wasiwasi na hasira ya utawala wa Kizayuni (Israel) kuhusu mchakato huu ni ishara wazi ya mafanikio na ushindi wa taifa la Iran. Kwa neema ya Mungu, njia hii itaendelea kwa nguvu,” amesema Rais Masoud Pezeshkian.

Rais amesifu juhudi kubwa zilizofanywa na wanachama wa timu ya mazungumzo ya Iran akiwemo kinara wake, Mohammad Baqer Qalibaf na Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araghchi na akasema, mafanikio hayo ya kidiplomasia ni kielelezo cha mafanikio makubwa kwa Jamhuri ya Kiislamu.

Amesema mafanikio ya kidiplomasia yametokana na mshikamano wa kupigiwa mfano, uwiano na uratibu miongoni mwa nguzo tatu kuu za utawala na vikosi vya jeshi la Iran.

Pezeshkian ameongeza kuwa utekelezaji kamili wa makubaliano hayo na uzingatiaji wa upande wa pili (Marekani) wa majukumu yake unaweza kufungua njia ya “kutatua matatizo mengi ya kikanda na kutengeneza mazingira mapya katika uwanja wa kimataifa.”

“Hatua zote zinachukuliwa ndani ya mfumo wa maslahi ya kitaifa na kwa kuzingatia mistari myekundu ya utawala wa Kiislamu,” amesisitiza Rais Pezeshkian.

Rais amesema miongozo na uungaji mkono wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Mojtaba Khamenei, imekuwa na nafasi kubwa katika kufikiwa mafanikio haya ya kidiplomasia.

“Kadiri tunavyosimama pamoja, hakuna nguvu yoyote ambayo itaweza kudhuru au kulemaza nchi hii,” Pezeshkian amesema.

Rais wa Iran ameongeza kwa kusema: Adui alidhani kwamba hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Iran ingetenganisha wananchi na serikali lakini taifa la Iran limetetea Mapinduzi ya Kiislamu, mfumo tawala wa Kiislamu na nchi yao kupitia hamasa yao kubwa na isiyo na kifani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *