
Barabara kuu ya ufukweni inayopita katika mji wa Zawiya nchini Libya, yapata kilomita 60 magharibi mwa mji mkuu Tripoli, imefungwa kabisa tangu Alkhamisi jioni baada ya kuzuka mapigano na ufyatulianaji risasi kati ya makundi yenye silaha ya eneo hilo.
Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha Al-Masar, wapiganaji kutoka Kikosi cha 103 kinachojulikana pia kwa jina la “Al-Silaa,” wamepigana na wapiganaji kutoka Kikosi cha Kwanza cha Usaidizi cha jimbo la Zawiya. Hakuna taarifa iliyoripotiwa kuhusu majeruhi na hakuna taarifa rasmi zilizotolewa kuhusu chanzo cha mapigano hayo.
Mapigano kama hayo yanatokea mara kwa mara nchini Libya. Hivi karibuni mapigano makali yalizuka upya katika eneo la Janzour, yapata kilomita 12 magharibi mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli, kati ya makundi hasimu yenye silaha ambayo yako chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) ya Waziri Mkuu Abdul Hamid Dbeibah.
Vyombo vya habari vya ndani ya Libya viliripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, mapigano yalianza wakati Kikosi cha Mahmoud Boujaafar kilipovamia makao makuu ya Brigedi ya Sita inayoongozwa na Munir Al-Sweih na kuzusha vita vikali ambavyo ndani yake silaha za kati na nzito zilitumika. Barabara kuu ya pwani ya kuelekea Zawiya na soko kuu la mboga ambayo hivi sasa imefungwa pia kutokana na mapigano makali.
Libya bado imegawanyika kati ya serikali mbili, moja ni ya Umoja wa Kitaifa GNU inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa inayotawala upande wa magharibi na nyingine ni serikali hasimu inayotawala upande wa mashariki mwa Libya ikiongozwa na Osama Hammad. Kuna mikono mingi ya nje inayochochea machafuko huko Libya. Serikali ya Osama Hammad inaungwa mkono na Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar.