Ghasia dhidi ya Waislamu nchini India zimeongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni.

Ongezeko la ukatili dhidi ya Waislamu nchini India hususan katika miaka michache iliyopita, linahusiana moja kwa moja na sera na mazungumzo ya chama tawala, ambacho kwa kuimarisha utaifa wa Kihindu, kimefungua njia ya ubaguzi na chuki dhidi ya walio wachache.

Katika miaka ya hivi karibuni, hususan mwaka jana 2024 na mwaka huu, jamii ya Waislamu wa India imekabiliwa na wimbi la vurugu zilizoratibiwa na zilizopangwa.

Ripoti nyingi zinaonyesha kuwa, ghasia hizi zina mizizi sio tu katika ngazi ya kijamii lakini pia katika ngazi ya kisiasa. Chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP), kilichoegemezwa kwenye itikadi ya utaifa wa Kihindu, kimefuata sera ambazo zimeweka pembeni ipasavyo dini a walio wachache, hasa Waislamu.

Sera hizi zimejumuisha mabadiliko ya sheria za uraia, vikwazo vya uhuru wa kidini, na uungwaji mkono wa kimyakimya kwa vikundi vya Wahindu wenye msimamo mkali.

Mnamo mwaka wa 2024, takwimu zilionyesha kuwa kiasi cha matamshi ya chuki dhidi ya Waislamu kiliongezeka kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea. Kulingana na ripoti ya India Hate Lab, idadi ya kesi zilizorekodiwa za matamshi ya chuki iliongezeka kutoka 668 mwaka 2023 hadi 1,165 mwaka 2024, ikionyesha ongezeko la 74%.

Nembo ya chama tawala nchini India cha Bharatiya Janata

Nukta muhimu zaidi ni kuwa, karibu asilimia 98 ya kesi hizi zililenga Waislamu. Ongezeko hili kubwa sio tu linaakisi anga ya mvutano wa kijamii nchini India, lakini pia linadhihirisha nafasi ya moja kwa moja ya viongozi wa chama tawala katika kuchochea mgogoro huu.

Vurugu hizo hazikuishia tu katika hatua ya maneno. Mnamo 2024, kulikuwa na ripoti nyingi za mashambulizi ya kimwili, uharibifu wa misikiti na maeneo ya kidini, mauaji ya chuki, na ubaguzi wa kupangwa. Vitendo hivi vilitokea katika majimbo mbalimbali ya India na kuonyesha kwamba, chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) ni jambo lilioenea.

Katika visa vingi, badala ya kuwaunga mkono wahasiriwa, vikosi vya usalama na polisi walipuuuza matukio hayo au hata walishutumiwa kwa kushirikiana na washambuliaji.

Mnamo 2025, Narendra Modi alipoanza muhula wake wa tatu kama Waziri Mkuu, hali ya Waislamu iliendelea kuwa mbaya. Ingawa kushindwa kwa chama tawala katika uchaguzi wa Bunge la Chini la India (Lok Sabha) kulifanya vyama vya upinzani na Wabunge Waislamu kupaza zaidi sauti zao, lakini sera za kupinga jamii za walio wachache zingali zinaendelea katika nchi hiyo.

Mabadiliko ya sheria za ndoa, vikwazo vya haki za uraia, na shinikizo za kijamii dhidi ya Waislamu ni miongoni mwa masuala ambayo yalizua maandamano makubwa. Maandamano haya yalidhihirisha kuwa walio wachache hawakuwa tayari kukaa kimya mbele ya sera za kibaguzi.

Waislamu nchini India wamekuwa wakishambuliwa na hata kuuawa na makundi ya Wahindu wenye misimamo ya kufurutu mpaka

Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, sera za chama tawala nchini India zimeegemezwa katika kuimarisha utambulisho wa Wahindu na kuwaondoa hatua kwa hatua walio wachache. Sera hizi sio tu zimesababisha kuongezeka kwa ghasia za moja kwa moja dhidi ya Waislamu lakini pia zimeleta mgawanyiko mkubwa katika kijamii.

Katika mazingira kama haya, Waislamu wanatambulishwa kama “wengine,” hatua ambayo inajenga msingi wa kuhalalisha unyanyasaji dhidi yao.

Kwa mtazamo wa kijamii, mwelekeo huu una matokeo ya hatari. Kwanza, hali ya kuaminiana kati ya jamii za kidini nchini India imeharibiwa sana. Pili, Waislamu, ambao wanaunda idadi muhimu na ya kuzingatiwa ya watu nchini India, wanahisi kwamba wamenyimwa haki zao za kimsingi.

Hisia hii ya kunyimwa inaweza kusababisha kukosekana kwa utulivu wa kijamii na hata athari za vurugu zaidi kwa muda mrefu. Tatu, sura ya India kama demokrasia kubwa zaidi duniani imechafuliwa kimataifa.

Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India

Hatimaye, ni lazima kusemwa kuwa kuongezeka kwa ghasia dhidi ya Waislamu nchini India mwaka 2024 na 2025 kulikuwa na matokeo ya moja kwa moja ya sera za chama tawala na mazungumzo ya kitaifa ya Kihindu.

Mwenendo huu sio tu unatishia usalama na haki za walio wachache, bali pia unahatarisha misingi ya demokrasia na kuishi pamoja kwa amani katika nchi hiyo.

Ijapokuwa maandamano ya walio wachache hususan Waislamu na mashinikizo ya kimataifa yanaweza kwa kiasi fulani kuzuia mchakato huu kuendelea, lakini ukweli ni kwamba bila ya mabadiliko ya kimsingi katika sera za serikali ya mrengo wa kulia ya India na kurejea katika misingi ya usawa na uadilifu, mustakabali wa Waislamu nchini India utaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *