
Mapigano makali yameendelea kushuhuudiwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo siku moja baada ya marais wa nchi hiyo kusaini makubaliano mapya ya amani mjini Washington Marekani.
Muungano wa waasi wa AFC/M23, unaoungwa mkono na Rwanda, ambao uliikamata miji miwili mikubwa mashariki ya Kongo mapema mwaka huu, umesema kupitia msemaji wake Laurence Kanyuka kuwa vikosi tiifu kwa serikali vinafanya mashambulizi. Msemaji wa jeshi la Kongo amesema makabiliano yanaendelea na kwamba vikosi vya Rwanda vinavyatua mabomu.
Kuendelea mapigano mashariki mwa DRC kumezusha maswali mengi hasa kwa kuzingatia kwamba, mapigano hayo yamezuka siku moja tu baada ya kutiwa saini mjini Washington Marekani makubaliano ya amani.
Marais Félix Tshisekedi wa DRC na Paul Kagame wa Rwanda walisafiri hadi mji mkuu huo wa Marekani kwa ajili ya utiaji saini huo, ambapo waliungana na viongozi kutoka mataifa mengine kadhaa ya Afrika.
Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo iliyofanyika mjini Washington, ilimpa Trump fursa nyingine ya kujitangaza kama msuluhishi na mleta makubaliano wa kimataifa. Rais huyo wa Marekani, ambaye ameonyesha mara kadhaa kiu yake ya kutaka atunukiwe Tuzo ya Amani ya Nobel, aliuita mkataba huo kama ushindi wa kidiplomasia.
Ikulu ya White House imeelezea makubaliano kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda kuwa ni “ya kihistoria,” yakitokana na hatua za miezi kadhaa ya upatanishi uliohusisha Marekani, Umoja wa Afrika na Qatar.