
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepasisha kwa wingi maazimio matano kwa ajili ya Palestina, ikiwa ni pamoja na kuongeza muda wa shirika la UNRWA, kulaani vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kuunga mkono haki za wakimbizi wa Kipalestina.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio kuhusu wakimbizi wa Kipalestina kwa kura 151 za ndio katika mkutano uliofanyika Ijumaa, kuonyesha uungaji mkono wa jamii ya kimataifa kwa haki za wakimbizi wa Kipalestina.
Azimio hilo lilipitishwa kwa kura 151 za ndio, 10 zilipinga na nchi zilijizuia kuupiga kura. Wanachama 10 wa Umoja wa Mataifa waliopiga kura dhidi yake ni Argentina, Fiji, Hungary, Israel, Macedonia Kaskazini, Palau, Papua New Guinea, Paraguay, Tonga na Marekani.
Azimio hilo linasisitiza jukumu muhimu la Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA katika kutekeleza programu muhimu za elimu, afya, misaada na huduma za kijamii kwa wakimbizi wa Kipalestina, pamoja na misaada ya kibinadamu ya kuokoa maisha katika maeneo yote ya operesheni nchini Jordan, Lebanon, Jamhuri ya Kiarabu ya Syria na eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu, hususan katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Baytul-Muqaddas Mashariki.
Azimio hilo pia linaonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu hali mbaya ya wakimbizi wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Baytul-Muqaddas Mashariki, hususan kuhusiana na usalama, ustawi na hali ya kijamii na kiuchumi.
Azimio hilo pia linaitaka Israel kuheshimu mamlaka ya UNRWA na kinga zake na kuchukua hatua za haraka kuhakikisha kuwa shughuli zake zinaendelea bila kipingamizi au vikwazo katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, ikiwemo Baytul-Muqaddas Mashariki.