Jana Desemba 5, 2025, Kituo cha Sanaa za Maonyesho cha John F. Kennedy kilikuwa jukwaa la maonyesho ya kisiasa na michezo.

Hafla ya droo ya mwisho ya mashindano ya Kombe la Dunia FIFA 2026, ambayo yamepangwa kufanyika Marekani, Canada na Mexico, iliadhimishwa na tukio la kushangaza: kukabidhiwa Tuzo ya Amani ya FIFA kwa Rais wa Marekani, Donald Trump.

Katika droo ya Kombe la Dunia 2026, Donald Trump amepewa Tuzo mpya ya Amani ya FIFA, suala ambalo limekosolewa vikali katika duru mbalimbali duniani. Uamuzi huo wa FIFA umeonekana kama jaribio la kuimarisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi na Trump, na wengi wameutambua kuwa ni “kujipendekeza na kujikomba kwa kiongozi huyo wa Marekani.”

Tuzo hiyo mpya, ambayo imepewa jina rasmi la “Tuzo ya Amani ya FIFA – Soka Inaunganisha Dunia”, imetolewa kwa mara ya kwanza kwa Trump na imesababisha wimbi kubwa la hisia kali. Katika hafla hiyo, Rais wa FIFA, Gianni Infantino alimpa Trump medali ya dhahabu kwa tabasamu lililoandamana na sifa mkemkem, akisema, “Unaweza kuvaa medali hii nzuri popote unapotaka.” Trump, akiwa na sura ya kuridhika kwa kufidia kushindwa kwake kupata Tuzo ya Amani ya Nobel, aliivaa medali hiyo shingoni mwake papo hapo, akiitaja kuwa ni ishara ya juhudi zake kwa ajili ya “amani duniani”.

Trump akivaa medali ya dhahabu ya FIFA

FIFA imeanzisha tuzo hiyo kama ubunifu wa kila mwaka na itakuwa ikitolewa kwa “watu binafsi ambao wamefanya juhudi kubwa na za kipekee kwa ajili ya amani na kuwaunganisha watu wa dunia.”

Trump, ambaye amekuwa akitumia vyombo vya habari na matuzo kama chombo cha kukuza chapa yake binafsi, amelitaja tukio hilo kuwa ni “wakati wa kihistoria kwa soka na amani” na ameahidi kuyafanya mashindano ya Kombe la Dunia 2026 kuwa “tukio kubwa zaidi la amani katika historia.” Hata hivyo watu wengi wameiona tuzo hiyo kuwa si heshima ya kweli, bali ni ubarakala na “kujikomba waziwazi” shirikisho la FIFA ili kuhakikisha mafanikio ya Kombe la Dunia 2026.

Kwa kitendo hicho, FIFA, shirika ambalo kwa kawaida husisitiza sera ya kutoegemea upande wowote kisiasa, imetumbukizwa katika mchezo wa kisiasa. Wakosoaji, wakiwemo wanaharakati wa haki za binadamu, wameutaja uamuzi huo kuwa wa kipuuzi na mchafu. Kwa mfano, mwanaharakati wa haki za binadamu Craig Gerard Mokhiber amesema katika mahojiano na televisheni ya Al Jazeera kwamba: “Baada ya miaka miwili ya ushiriki wa FIFA katika mauaji ya kimbari ya Palestina, Infantino na washirika wake sasa wamebuni tuzo mpya ya amani ili kujiunga na Trump.” Ukosoaji huo unarejea nyuma katika uhusiano mkubwa wa Gianni Infantino na Donald Trump, ambao ulianza tangu Marekani ilipofuzu kura ya kuandaa mashindano ya Kombe la Dunia FIFA 2026 na unajumuisha mikutano ya mara kwa mara wa wawili hao na kuungana mkono pande hizo mbili.

Vyombo vya habari vya Magharibi pia vimetumia fursa hiyo kudhihaki hatua hiyo ya FIFA. Gazeti la The Guardian limeandika katika makala ya kejeli kwamba: “Trump ashinda Tuzo ya Amani ya FIFA – je, VAR inaweza kuibatilisha?” Gazeti hilo limeelezea hafla ya droo ya mwisho ya mashindano ya Kombe la Dunia FIFA 2026 huko Marekani kuwa ni onyesho la bei rahisi lililobuniwa kwa ajili ya kumfurahisha Trump.

Hata ndani ya Marekani kwenyewe, Wademokrati wameita hatua hiyo kuwa ni “mchezo wa kisiasa wa FIFA kwa ajili ya kuishawishi Washington.” Gazeti la USA Today limeripoti kwamba, Trump alikuwa “mshindi” wa tuzo hiyo tangu miezi kadhaa iliyopita, jambo ambalo linaimarisha tuhuma kwamba “ilibuniwa” hivyo. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, hakukuwa na ushindani wowote kwa ajili ya tuzo hiyo, na Trump ndiye aliyekuwa mgombea pekee.

Ukosoaji huu unatokana na historia tata ya FIFA; shirika ambalo limekabiliwa na kashfa za ufisadi na tuhuma za ubaguzi wa rangi na sasa limehatarisha zaidi uaminifu wake kwa kuingia katika ulingo wa siasa.  

Hatimaye inatupasa kusema kuwa, kumpa Trump Tuzo ya Amani ya FIFA ni ishara ya kupingana michezo na siasa badala ya kuwa nembo ya umoja na mshikamano. Kwa kupewa medali hiyo, Trump ameongeza kwenye mkusanyiko wake binafsi wa tuzo, lakini FIFA imeibua maswali mazito kuhusu uhuru na kujitawala kwake. Je, tuzo hii ya kila mwaka itakuwa chombo cha diplomasia ya michezo au nembo ya ufisadi wa kisiasa? Muda, na labda utendaji wa FIFA katika miaka ijayo, utaweka wazi jibu la swali hili.

Kilicho hakika ni kwamba, tukio hili limehamisha mjadala kutoka uwanja wa mpira wa miguu hadi uwanja wa kimataifa na kuonyesha kwamba, siasa zipo wakati wote katika ulimwengu wa michezo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *