Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imewatuhumu wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kuwa wameua raia 79 wakiwemo watoto 43 katika mauaji ya halaiki kwenye mji wa Kalogi katika jimbo la Kordofan Kusini.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imeeleza kuwa mashambulizi hayo ni sehemu ya kampeni inayoendelea ya mauaji ya kimbari ya wanamgambo wa RSF dhidi ya jamii za Wasudani. Mashambulizi ya siku ya Alkhamisi yaliua raia 79 wakiwemo watoto na wanawake 43. 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imesema kuwa wanamgambo wa RSF waliilenga kwa roketi shule ya watoto wadogo (chekechea) kwa lengo la kuua idadi kubwa ya watoto. 

“Wakati wenyeji walipokimbilia kuwasaidia majeruhi, wanamgambo wa RSF waliishambulia tena shule hiyo ya chekechea na kufanya mauaji zaidi ikiwa ni pamoja na kuua watoto ambao walinusurika katika shambulio la kwanza,” imeongeza taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan. 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa wanamgambo wa RSF waliwakimbiza majeruhi na madaktari waliokuwepo hospitali  na hivyo kuifanya idadi ya vifo kufikia 79 na kujeruhi wengine 38. 

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imeongeza kuwa: Mashambulizi hayo “ni ushahidi mpya kwamba wanamgambo wa RSF wanatafsiri kimya cha jamii ya kimataifa kama kichocheo na idhini ya kuendelea kufanya ukatili.”

Wakakti huo huo Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, ametoa indhari kuhusu hatari ya kuzuka wimbi jipya la ukatili katika eneo la Kordofan, Sudan, baada ya kushadidi mapigano kati ya Jeshi la Sudan (SAF), waasi wa RSF na kundi la Harakati ya Ukombozi wa Wananchi wa Sudan- Kaskazini (SPLM-N).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *