Waziri wa Mambo ya Nje wa Ira amesema iwapo Marekani itabadili mkondo wake, Iran nayo itakuwa tayari kupata matokeo ya haki na usawa.

Katika mahojiano maalum na Shirika la Habari la Kyodo la Japan, Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza ulazima wa pande zinazofanya mazungumzo kuwa tayari kupata “matokeo ya haki na yenye uwiano” katika mchakato wa mazungumzo hayo.

Kuhusu matarajio ya mazungumzo hayo, Araqchi alisema kuwa maendeleo ya mazungumzo hayo yanategemea mtazamo wa Marekani.

Araqchi ameongeza kuwa, “Iwapo Marekani itabadilisha mtazamo na mwenendo wake na kuwa tayari kufikia makubaliano ya uwiano na manufaa kwa pande zote mbili, sisi pia tuko tayari.” Pia amesisitiza kuwa uzoefu wa Iran katika mazungumzo na Marekani haujawa “mzuri.”

Akizungumzia kufungamana Iran na Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alibainisha: “Iran ni mwanachama mwenye kuheshimu mkataba wa NPT na, kama ilivyo Japan, ina haki ya kunufaika na teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani.” Pia aliongeza kuwa Japan, ikiwa ni mwanachama aliyejitolea katika mkataba huo, pia nayo ina haki ya matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amewahi kusisitiza mara kadhaa kwamba, ili kupiga hatua kuelekea kwenye mustakabali, ni lazima kwanza tufikie kwenye uelewa wa pamoja juu ya ukweli kwamba, kimsingi, hakuna kitu kinachoitwa “chaguo la kijeshi,” achilia mbali “suluhisho la kijeshi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *