Serikali ya Uhispania imetangaza kuwa, ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaofanywa na utawala wa Israel katika maeneo ya Wapalestina ni kinyume na sheria za kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania José Manuel Álvarez amesema kuwa: “Hakuna kazi maalumu kwa vikosi vya kimataifa huko Gaza. Taifa la Palestina lazima liweze kuishi kwa amani.”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania ameeleza pia kuwa, “Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, na sisi na Wazungu hatutatambui unyakuzi wowote. Ujenzi wa vitongoji vya walowezi (vitongoji vya walowezi wa Kizayuni) lazima ukomeshwe kwa sababu ni kinyume cha sheria za kimataifa.” Utawala dhalimu wa Israel unaendelea kupora ardhi za Wapalestina na kuharibu nyumba zao kwa shabaha ya kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni lengo lake kuu likiwa ni kutaka kubadilisha muundo wa kijiografia wa maeneo ya Palestina na kuimarisha ukandamizaji wake katika maeneo hayo.

Katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hususan katika Msikiti wa al-Aqswa vimeongezeka mno.

Madola ya Magharibi yamekuwa yakikosolewa kutokana na himaya na uungaji mkono wao kwa utawala ghasibu wa Israel na hata wengi wanaamini kuwa, himaya hiyo ndiyo inayoupa kiburi utawala huo ghasibu cha kuendeleza uharibifu na jinai zake huko Palestina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *