Serikali ya Nigeria imefanikisha kuachiliwa huru watoto 100 wa skuli waliotekwa nyara mwezi uliopita katika Jimbo la Niger. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na televisheni ya Channels Television jana Jumapili.

Hata hivyo Channels Television haikutoa maelezo zaidi kuhusu namna wanafunzi hao walivyoachiliwa.

Chama cha Wakristo cha Nigeria kilitangaza hapo kabla kuwa watoto 303 na wafanyakazi 12 wa skuli walitekwa nyara tarehe 21 Novemba na watu wenye silaha katika skuli ya dakhalia ya Kanisa Katoliki ya St Mary’s huko Papiri.

Wanafunzi 50 walifanikiwa kutoroka katika masaa yaliyofuata, lakini tangu wakati huo hakujakuwa na taarifa kuhusu waliko au hali ya watoto wengine. Imeelezwa kuwa baadhi yao walikuwa na umri wa miaka sita tu.

Ikulu ya Rais wa Nigeria kupitia msemaji wake Sunday Dare imethibitisha kuachiliwa baadhi ya wanafunzi waliokuwa wametekwa nyara

Aidha, chanzo kimoja kimevieleza vyombo vya habari kwamba waathirika walioachiliwa “watakabidhiwa kwa serikali ya Jimbo la Niger leo Jumatatu”.

Shambulio dhidi ya skuli jimboni Niger lilidhihirsha ukosefu wa usalama nchini Nigeria, ikiwa imepita zaidi ya miaka 10 tangu ulipotokea utekaji nyara wa wasichana wanaokaribi 300 kwenye mji wa Chibok ulioko kusini mwa jimbo la Borno kaskazini mashariki ya nchi hiyo…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *