
Umoja wa Mataifa leo umezindua ombi la misaada ya kibinadamu duniani la dola bilioni 33, ukiomba nchi na wadau kote ulimwenguni kuongeza msaada kwa mamilioni ya watu wanaokabiliwa na migogoro kutokana na vita, majanga ya tabia nchi, miripuko ya maradhi, na njaa.
Lengo la haraka la ombi hilo ni kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa watu milioni 87 kwa dola bilioni 23 za awali, huku lengo la 2026 likiwa kusaidia watu milioni 135 katika nchi 50.
Mkuu wa Kuratibu Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher amesema: “Ombi hili linaonesha wapi tunapaswa kuelekeza nguvu zetu pamoja kwanza, maisha kwa maisha”.
Uzinduzi wa ombi hili umefanyika baada ya mwaka mgumu wa 2025 ambapo ufadhili wa misaada ya kibinadamu umeshuka hadi dola bilioni 12, kiwango cha chini zaidi katika muongo mmoja, na kusababisha watu milioni 25 kushindwa kufikiwa ikilinganishwa na 2024.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mpango mkubwa zaidi wa msaada binafsi ni kwa Eneo la Palestina lililokaliwa kimabavu na utawala wa kizayuni wa Israel, likihitaji dola bilioni 4.1 kusaidia watu milioni 3 waliokumbwa na vurugu na uharibifu mkali.
Nchi ya Sudan, yenye hali mbaya zaidi ya wakimbizi duniani, inahitaji dola bilioni 2.9 kwa watu milioni 20. Mpango wa Syria, ambao ni wa kikanda mkubwa zaidi, unahitaji dola bilioni 2.8 kusaidia watu milioni 8.6…/