
Serikali ya Kenya imekanusha madai kwamba maelezo ya kibinafsi ya matibabu ya Wakenya yataanza kutumwa kwa serikali ya Marekani chini ya mkataba mpya wa afya kati ya Nairobi na Marekani.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Katika taarifa siku ya Jumapili, Waziri wa Afya nchini Kenya Aden Duale alisema makubaliano hayo yanaeleza wazi kwamba Nairobi itabaki na umiliki wa data za raia wake.
Aidha Duale alisema katika makubaliano hayo, serikali ya Kenya itakuwa inashiriki na Marekani takwimu za matokeo ya vipimo vya maradhi na rasilimali zitakazotumika katika maabara, na wala sio maelezo ya kibinafsi kama vile majina, nambari za vitambulisho, nambari za simu, au faili za matibabu.
Waziri huyo ametoa hakikisho kuwa makubaliano hayo yamezingatia miongozo ya kisheria ya Katiba, na sheria zinazoilinda maelezo ya kibinfasi ya wakenya ikiwemo Sheria ya Ulinzi wa Data 2019.
Mkataba huo uliotiwa saini jijini Washington Alhamisi wiki iliyopita, utawezesha serikali ya Marekani kuwekeza Dola bilioni 2.5 katika taasisi za afya za Kenya katika miaka 5 ijayo.