Hatua hii inalenga kutoa msaada wa kibinadamu na kuimarisha mifumo inayofanya uhamiaji kuwa salama, wa utaratibu na wa kuheshimu haki.
Kupitia ombi hilo, IOM inataka kuhakikisha msaada unawafikia wahitaji kwa wakati na kuboresha mifumo ya ulinzi kwa watu wanaohama duniani.
“Kila siku, watu wanaondoka makwao wakitafuta utulivu au fursa bora, kupitia ombi hili tunajenga dira ya pamoja ambapo msaada wa kibinadamu unawafikia watu kabla migogoro haijazidi, njia salama zinachukua nafasi ya safari hatarishi, na jamii zinaimarishwa badala ya kulemewa. Uwekezaji huu haufikii tu mahitaji ya leo, unaunda mustakabali bora, wa kibinadamu na wenye matumaini kwa wote.” amesema Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Amy Pope.
Katika MRC, wafanyakazi wa IOM kama vile Kadija wanasaidia watoto wahamiaji na watu wazima katika kujenga uwezo wa kustahimili ustahimilivu kupitia sanaa na uchezaji baada ya uzoefu mgumu.
Migogoro inachochea uhamiaji
Kwa mujibu wa IOM uhamiaji unaendelea katika dunia inayokabiliwa na misururu ya migogoro. Mtu mmoja kati ya wanne anaishi katika mazingira tete yenye mivutano, migogoro au majanga. Kufikia mwisho wa 2024, watu milioni 83.4 walikuwa wameyakimbia makazi yao kutokana na migogoro, vurugu na majanga, huku dharura mpya zikiendelea kuzidi uwezo wa jamii kukabiliana nazo. Katika muktadha huu, kurejea kwa hiari kwa njia salama na yenye heshima pamoja na ujumuishaji endelevu ni muhimu katika kuimarisha uthabiti na kusaidia maendeleo ya muda mrefu.
Janga la tabianchi lnaongeza shinikizo. Mwaka 2024, majanga yaliwakosesha makazi watu milioni 9.8, ikiwa ni ongezeko la asilimia 27 kutoka 2023.
Hasara za kiuchumi duniani zilifikia Dola bilioni 242. Uhamiaji usio wa kawaida uliendelea kuwa hatarishi, huku zaidi ya vifo na watu 5,500 kupotea vikirekodiwa katika mwaka 2025.
Wakati huohuo, Shirika hilo limesema uhamiaji unachochea mnepo, ubunifu na fursa. Zaidi ya watu milioni 304 ni wahamiaji wa kimataifa, wakiwemo wafanyakazi milioni 168 wanaoendesha sekta muhimu na kusaidia jamii duniani kote.
Bi. Pope amesema wahamiaji wanaimarisha uchumi, kutoa huduma hospitalini, kuendeleza kilimo na kuendesha biashara ndogo ndogo.
Fedha zinazotumwa kutoka nje na wahamiaji zilifikia Dola za Marekani bilioni 883 mwaka 2024, zikionesha jinsi uhamiaji salama na wenye heshima unavyokuza maendeleo na uthabiti.
Katika doria tembezi karibu na Obock, Kadija na wafanyikazi wengine wa IOM wanawafikia wahamiaji kwenye korido hatari kwa huduma ya haraka ya matibabu.
Kipaumbele kwa uhamiaaji
Katika mazingira ambapo mahitaji yanaongezeka na rasilimali ni haba, ombi la IOM linataka upangaji wa kipaumbele ulio makini, ufadhili rahisi na mifumo inayofanya kazi kwa ufanisi ili kukidhi mahitaji ya dharura na kusaidia suluhu za muda mrefu.
Ombi hili linaendana na nguzo kuu tatu za shirika limesema shirika la IOM ambazo ni , kuokoa maisha na kulinda watu wanaohama, kuendesha suluhu za kudumu kwa waliokoseshwa makazi, na kuwezesha njia salama na za kawaida za uhamiaji.
IOM inataka Dola bilioni 1.5 kulinda watu walioko katika harakati za uhamaji ikiwa ni pamoja na makazi ya muda, maji safi, huduma za afya, ulinzi na huduma zingine muhimu.
Hii inajumuisha huduma za afya zinazohamishika katika maeneo yenye migogoro, makazi ya dharura baada ya majanga ya tabianchi, na kuimarisha misururu ya usambazaji wa misaada.
Takribani Dola bilioni 1.3 zitaelekezwa katika kuunga mkono njia salama na za kawaida za uhamiaji ikiwemo kuimarisha uhamaji wa wafanyakazi, kulinda haki za wahamiaji na kuweka mifumo inayowezesha manufaa ya kijamii na kiuchumi.
Kupitia ombi hili IOM inahimiza serikali, wafadhili na wadau wake kuongeza juhudi. Shirika hili linatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuwekeza katika uthabiti, usalama na hadhi ya watu wanaohamahama na jamii zinazowapokea, kuhakikisha uhamiaji unakuwa kichocheo cha maendeleo endelevu kwa wote. Amehitimisha bi Pope.