masTaarifa iliyotolewa jijini New York Marekani na msemaji wa Katibu Mkuu wa UN António Guterres amesema kuwa ameshtushwa sana kusikia kuwa mashambulizi hayo ya tarehe 4 Desemba yalipiga shule ya chekechea ya watoto na hospitali katika eneo la Kalogi, ambako majeruhi walikuwa wakipatiwa matibabu.

Akiunga mkono wasiwasi huo, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, naye ametoa taarifa yake na kusema kuwa Hospitali ya Kalogi imelengwa angalau mara tatu, na kusababisha vifo vya watu 114, wakiwemo watoto 63.

Wito wa kuchangia damu na msaada wa haraka

Dkt. Tedros amesema manusura wa mashambulizi hayo wamehamishiwa Hospitali ya Abu Jebaiha katika eneo la Kordofan Kusini kwa matibabu, na “mito wa dharura unatolewa kwa uchangiaji wa damu na msaada mwingine wa kitabibu”.

“Inasikitisha kwamba wahudumu wa afya na vikosi vya zima moto walishambuliwa walipokuwa wakijaribu kuwahamisha watoto waliojeruhiwa kutoka shule ya chekechea kwenda hospitali,” aliongeza.

Siku hiyo hiyo ya mashambulizi, msafara wa misaada nao ulilengwa katika eneo la Kordofan Kaskazini. Msafara huo ulikuwa ukisafirisha vifaa muhimu vya kuokoa maisha kwenda Darfur Kaskazini wakati uliposhambuliwa, na kumjeruhi vibaya dereva wa lori la Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).

“Katibu Mkuu analaani shambulio hili dhidi ya shughuli za kibinadamu wakati mahitaji yakiwa makubwa kuliko wakati mwingine wowote,” imesema taarifa yake.

Mateso makubwa kwa raia

Mashirika ya kibinadamu yanaonya hali nchini Sudan inaendelea kuwa mbaya sana kwa mamilioni ya watu waliokwama katikati ya mapigano makali kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF).

Katika eneo la Kordofan ya Kati, hali mbaya inazidi kuwa mbaya zaidi huku vifaa vya kuokoa maisha vikiisha, wakati njaa kali imethibitishwa katika mji mkuu wa Kordofan Kusini, Kadugli.

“Huku mapigano yakizidi kupamba moto, ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ulioonekana huko El Fasher miezi ya hivi karibuni, pamoja na ripoti za uvunjaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu, havipaswi kurudiwa katika eneo la Kordofan,” msemaji wa Katibu Mkuu alisisitiza.

Aidha, kufuatia taarifa za kuendelea kwa ushiriki wa mataifa ya kigeni katika mgogoro wa Sudan, “Katibu Mkuu anatoa wito kwa mataifa yote yenye ushawishi juu ya pande kinzani kutumia nguvu yao kuzilazimisha kusitisha mapigano mara moja na kusimamisha mtiririko wa silaha” zinazoendeleza vita hivyo.

“Katibu Mkuu anarejea wito wake kwa pande zote kukubali kusitisha mapigano mara moja na kurejea kwenye mazungumzo ya kuelekea usitishaji wa kudumu wa mapigano na mchakato wa kisiasa wa Sudan unaomilikiwa na Wasudan wenyewe. Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia hatua za dhati za kusitisha vita na kuweka njia kuelekea amani ya kudumu.”

Wito wa Kamishna wa Haki za Binadamu

Taarifa hizi zinakuja baada ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, kusema kuwa ana hofu ya “wimbi jingine la ukatili” nchini Sudan.

Tangu mwishoni mwa mwezi Oktoba, mamia ya raia wameuawa na makumi ya maelfu kukimbia mashambulizi ya angani, mabomu na mauaji. Zaidi ya watu 45,000 wamekimbia makazi yao wakitafuta usalama ndani na karibu na eneo la Kordofan.

“Kutoa nafasi salama kwa wanaokimbia njaa, vifo na uharibifu ni muhimu na ni haki ya msingi ya kibinadamu,” ofisi ya Kamishna ilisema.

Katika wito kwa “hatua za dharura za kidiplomasia,” Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa WFP Carl Skau alisisitiza kuwa kunahitajika umakini mkubwa zaidi ili kuzuia ukatili zaidi na kurejesha hali kutokana na njaa inayoenea.

Zaidi ya watu milioni 30 nchini Sudan sasa wanahitaji msaada wa kibinadamu, huku zaidi ya watu milioni tisa wakiwa wamekimbia makazi yao ndani ya nchi tangu mapigano yaanze mwezi Aprili 2023 kati ya SAF na RSF.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *