
Umoja wa Mataifa upo nchini Sudan kuhakikisha wanasaidia wananchi wa taifa hilo kwa mahitaji mbalimbali hata wakati wa kipindi hiki kigumu ambapo makundi yenye silaha yakipingana na kusababisha vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Moja ya shirika lililopo nchini Sudan ni lile la mpango wa chakula duniani WFP ambalo pamoja na mambo mengine linatoa msaada wa chakula cha moto, yani kuna kuwa na majiko maalum ya jumuiya katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ambayo WFP hutoa vyakula, majiko na vifaa vyote muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata mlo.
Mathalani huko Khartoum WFP wanamajiko takriban 200 ya jumuiya ambayo mbali na kutoa chakula cha moto lakini kuna kundi muhimu ambalo ningependa hii leo tuliangazie.
Wapishi, wapakuaji na wote wanaofanya juhudi kuhakikisha wananchi wanapata mlo. Hawa ni wananchi wa kawaida ambao nao wanakumbwa na madhila yote yaletwayo na vita lakini wanajitolea kusaidia wananchi wenzao. Mmoja wa watu hawa muhimu ni kijana Sufyan.
“Mimi ninajitolea katika jiko la kupika supu lililoko Al- Jerif Mashariki, mashariki mwa Karkoj, watu wa kujitolea hapa tunatoa usaidizi mbalimbali. Majiko haya yakutoa chakula cha moto yalianzishwa kwa haraka wakati ambao wananchi walikuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa na yamekuwa msaada muhimu sana.”
Je wanafanya kazi muda gani?
“Muda mwingine tunakesha hapa ili tuweze kuhakikisha tunawapatia wananchi kifungua kinywa asubuhi. Isingekuwa msaada huu wa WFP basi watu wasingalikuwa na msaada huu mkubwa. Nawashukuru kwa juhudi zao.”
Hongera sana Sufyan na wote mnaojitolea katika kuhakikisha mnawasaidia wananchi wenzenu wa Sudan.