Shirika la Human Rights Watch limesema serikali ya Tanzania inapaswa kuusimamisha msako wake na kuwaachilia mara moja wote waliokamatwa kiholela.
Matamko hayo yametolewa huku nchini Tanzania kukitarajiwa kufanyika maandamano siku ya Jumanne Desemba 9 siku ambayo Tanzania bara husherehekea siku ya Uhuru wake.
Serikali imefuta sherehe rasmi za siku hiyo ya Uhuru baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza kwamba fedha za sherehe hizo zitumike kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa wakati wa machafuko ya Oktoba 29 wakati wa uchaguzi.
Mtafiti mkuu wa shirika la Human Rights Watch kanda ya Afrika Oryem Nyeko, amesema:
“Serikali ya Tanzania inajenga msingi wa hali ya vitisho na hofu iliyokuwepo kabla ya uchaguzi ili kuzuiakufanyika maandamano zaidi.” Oryema amesema Mamlaka zinapaswa kukomesha ukandamizaji na ziheshimu haki ya Watanzania kuhusu kutoa maoni yao kwa amani.”
Sherehe rasmi za uhuru zaahirishwa
Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba ametangaza kuwa hakutakuwa na sherehe rasmi mwaka huu. Serikali ya Tanzania imewashauri raia wote ambao hawatakuwa na dharura mnamo Desemba 9 kuitumia siku hiyo kwa ajili ya mapumziko, isipokuwa wale ambao majukumu yao ya kazi yanawalazimu wawe katika vituo vyao vya kazi.
Polisi imesema, maandamano yoyote yatakuwa kinyume cha sheria kwa kuwa mamlaka haijapokea taarifa yoyote rasmi kutoka kwa waandaaji wa maandamano hayo. Kauli hiyo imesisitizwa zaidi na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania George Simbachawene:
“Maandamano hayo ni haramu, hayaruhusiwi na tutumie nafasi hii kuwaomba sana wale wote ambao wanashabikia,wale wote ambao wanaona wameichoka amani,wale wanaoona kwamba mateso tuliyoyapata katika kipindi hiki hayatoshi na wanataka kutuongezea mengine. Tuwaombe sana, maandamano yanapokuwa hayana kibali na hayapo kwa mujibu wa sheria hayakubaliki na kwa hivyo vyombo vyetu vya usalama vitayadhibiti.”
Ulinzi umeimarishwa kwa kuwekwa vikosi vya polisi na wanajeshi walioonekana kando ya barabara kuu katika mji mkuu wa kibiashara Dar es Salaam na kwenye mji wa kaskazini mwa wa Arusha.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema hata kabla ya maandamano yaliyopangwa kufanyika Desemba 9, mamlaka ilionekana kuzidisha unyanyasaji kwenye mitandao ya kidijitali na ufuatiliaji wa wanaharakati.
Kampuni ya teknolojia ya Meta, katika ripoti yake ya Vizuizi vya Maudhui ya mwezi Desemba imeripoti kwamba imeondoa na kuzuia ufikiaji wa maudhui nchini Tanzania baada ya kuombwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano nchini humo kuzuia akaunti tatu za Instagram kwa madai kuwa zinakiuka sheria za taifa hilo la Afrika Mashariki.
Shirika la Human Rights Watch limesema serikali ya Tanzania inapaswa kufikiria upya na kuchukua hatua za kuhakikisha uwajibikaji bila upendeleo kuhusu madai ya mauaji yanayohusiana na uchaguzi, vipigo, na mashambulizi kutoka kwa vikosi vya usalama na watu wasiojulikana, kuhakikisha ushiriki mpana katika uchunguzi wa yaliyotokea nchini Tnazania, na kuwawajibisha wale wote waliohusika.
Sheria za kimataifa
Sheria za Tanzania na za kimataifa zinatakiwa kuhakikisha uhuru na kulinda haki ya kila mtu ya kutoa maoni yake kwa uhuru, kujumuika, na kukusanyika kwa amani bila vikwazo vyovyote visivyo vya lazima.
Vyombo vya kikanda, ikiwa ni pamoja na Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika na Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu, vinapaswa kuzihimiza mamlaka za Tanzania kutekeleza majukumu haya, kukomesha vitendo vya kuwanyanyasa wakosoaji, na kutoa ushirikiano katika uchunguzi huru, unaozingatia haki kuhusu ukiukwaji wa haki ulitokea baada ya uchaguzi.
