Kwa mara ya pili tangu PASTEF iingie madarakani mwezi Machi 2024, mkuu wa serikali ya Senegal ameonyesha nia yake katika uchaguzi ujao wa urais. “Hakuna kinachoweza kunizuia kuwa mgombea!” alitangaza siku ya Jumapili, Desemba 7. Kauli hii inakuja huku swali la ustahiki wake likiibuka tena katika mjadala wa umma na huku viongozi wawili wakuu serikalini wakionyesha dalili za mvutano.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Na mwandishi wetu huko Dakar, Léa-Lisa Westerhoff

Nchini Senegal, Waziri Mkuu Ousmane Sonko ametangaza kwamba anakusudia kikamilifu kuwa mgombea katika uchaguzi wa urais wa 2029. Siku ya Jumapili, Desemba 7, mkuu wa serikali ya Senegal alitumia fursa ya siku ya kuwakumbuka waathiriwa wa maandamano yaliyotokea kati ya mwaka 2021 na 2024 kufafanua nia yake ya uchaguzi ujao. “Hakuna kinachoweza kunizuia kuwa mgombea!” Alitangaza katika hafla iliyoandaliwa na chama chake, akiweka wazi msimamo wake: iwe ni kwa uchaguzi wa urais, wa wabunge, au wa serikali za mitaa, uamuzi wa kushiriki au kutoshiriki unategemea yeye pekee.

Tangu PASTEF ilipoingia madarakani mwezi Machi 2024, hii ni mara ya pili kwa mkuu wa serikali kuelezea hadharani matarajio yake ya uchaguzi ujao wa urais. “Hakuna kinachoweza kunizuia kuwa mgombea,” alisema maraya kwanza mnamo mwezi Julai mwaka huu katika video iliyorushwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Kuwahakikishia wafuasi wa PASTEF”

Kulingana na mwandishi wa habari Assane Samb, kauli hii ya Ousmane Sonko inalenga hasa “kuwahakikishia wafuasi wa PASTEF” kwani swali la ustahiki wake limeibuka tena katika mjadala wa umma katika wiki za hivi karibuni. Sababu? Uamuzi wa Mahakama Kuu mwezi Julai mwaka huu wa kumhukumu kifungo cha miezi sita jela  na kulipa faranga milioni 200 za CFA kama fidia kwa kashfa hii. Hukumu hii, katika kesi ya kwanza, ilimzuia kugombea katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2024…

Ingawa chama cha PASTEF kinajaribu kutuliza umma, kikidai kwamba kashfa hiyo iko chini ya sheria ya msamaha iliyopitishwa mwaka jana, baadhi ya wataalamu wa sheria wanabainisha kwamba sivyo ilivyo, kwani uamuzi wa Mahakama Kuu ulikuwa wa mwisho baada ya kupitishwa kwa sheria hiyo. Kwa vyovyote vile, “hakuna anayeweza kusema ni nani atakayekuwa mgombea mwaka wa 2029,” anaonya mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, kwani Baraza la Katiba litakuwa na jukumu la kuthibitisha wagombea hao kwa uhuru.

Lakini ikiwa Ousmane Sonko amerejelea tena matarajio yake ya urais, inaweza pia kuwa ni kutokana na “mvutano wa sasa kati ya Rais Bassirou Diomaye Faye na Waziri Mkuu wake,” kulingana na mchambuzi wa masuala ya sheria Daouda Mine, pamoja na kuwepo kwa “kutokubaliana” kati ya wakuu hao wawili katika serikali. Hakika, mkuu wa nchi hivi majuzi alifufua muungano uliounga mkono ugombea wake mwaka wa 2024, bila kufichua nia yake mwenyewe…

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *