
Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limewasilisha malalamiko rasmi kwa Shirikisho la Soka Duniani, FIFA, dhidi ya hatua isiyo ya kimichezo ya kamati ya maandalizi ya Kombe la Dunia mjini Seattle, Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, kamati ya mji ambao ni mwenyeji wa mechi kati ya Iran na Misri itakayochezwa Juni 26, 2026 katika uwanja wa Lumen Field, imeamua kuwa nara ya mechi hiyo itakuwa “Mchezo wa Kuheshimu Watu Wenye Uhusiano wa Jinsia Moja.”
Iran imesema hatua hiyo haina uhusiano na michezo na imekiuka kanuni za FIFA ambazo zinakataza kauli na vitendo vya kibaguzi, kijinsia au kidini. Aidha, imeelezwa kuwa kwa kuwa timu mbili za mataifa ya Kiislamu zinakutana, uamuzi huo wa wenyeji haukubaliki kwa upande wa Iran.
Timu ya taifa ya Iran, chini ya kocha Amir Qal’eh-Noei iko katika kundi ambalo pia linajumuisha timu za Ubelgiji na New Zealand.