
Uchunguzi wa bunge la Kenya kuhusu makosa na ukiukaji uliofanywa na Kikosi cha Mafunzo cha Jeshi la Uingereza nchini Kenya (BATUK) umeibua wito wa muda mrefu wa kuhoji mienendo ya majeshi ya kigeni barani Afrika.
James Mwangi, mwanzilishi wa African Centre for Corrective and Preventive Action, aliambia Sputnik Africa kwamba: “Hatua ya bunge kuchunguza shughuli za mafunzo ya Jeshi la Uingereza… ni mafanikio makubwa… ni mwito wa tahadhari kwamba mabunge mengine ya Afrika yanapaswa kuchukua hatua na kusimamia kambi hizi.”
Mwangi alieleza kuhusu miongo ya tuhuma za ukiukaji, unyanyasaji wa kijinsia, uchafuzi wa mazingira, na uzembe wa kifo kutokana na mabomu yaliyosalia bila kulipuka. Alilaani matumizi ya fosforasi nyeupe, silaha iliyopigwa marufuku, katika “mazingira nyeti yenye jamii za wafugaji, binadamu na misitu asili,” akisema ni “uchafuzi wa udongo wetu… mimea yetu… maisha yetu na vyanzo vya maji.”
Alisisitiza kuwa matokeo ya uchunguzi wa bunge lazima yapelekee hatua za haraka. Amesema “silaha hatari sana zilizobaki ardhini bila kulipuka wakati wa mafunzo ya kijeshi”, tayari zimesababisha vifo kwa watu na mifugo.
Ripoti ya uchunguzi ya bunge la Kenya imewatuhumu wanajeshi wa Uingereza walioko nchini humo kwa unyanyasaji wa mara kwa mara wa kingono, mazoezi yasiyo salama na ukiukaji wa mazingira. Ripoti hiyo imebainisha kuwa mienenendo hiyo imewafanya wanajeshi hao ajinabi kujiona kama “kikosi vamizi”.
Ripoti hiyo iliyotolewa wiki hii na Kamati ya Ulinzi na Mahusiano ya Nje ya Bunge la Kenya imeakisi hasira na malalamiko mkabala wa vitendo vinavyofanywa na Kitengo cha Mafunzo cha Jeshi la Uingereza nchini Kenya (BATUK), ambacho hupokea maelfu ya wanajeshi wa Uingereza kila mwaka.
Kesi maarufu zaidi inahusu mauaji ya Agnes Wanjiru mwenye umri wa miaka 21 yaliyojiri mwaka 2012 karibu na kambi ya mafunzo ya Waingereza huko Nanyuki. Mshukiwa mkuu, mwanajeshi wa Uingereza kwa jina la Robert Purkiss, alikamatwa nchini Uingereza mwezi uliopita baada ya kampeni ya miaka kadhaa ya familia ya Wanjiru na wanaharakati wa Kenya.
Katika ripoti hiyo, wabunge wa Kenya pia wamewasilisha ushahidi wa utupaji taka zenye sumu na uharibifu mwingine wa mazingira.