Sote tunafahamu nchi yetu imepita katika kipindi cha siku takribani 40 tangu vurugu za Oktoba 29, 2025 lakini ni muhimu sana kama Taifa huru, tukatafakari faida na hasara za utawala wa kisheria, kiuchumi, kijamii na ‘lockdown’ au kuzuiwa ndani.

Hakuna ubishi kuwa vurugu za siku ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani wa Oktoba 29, 2025 umesababisha vifo vya Watanzania ambao idadi yao bado ni siri ya watawala, majeruhi na kuharibu mali za Serikali na za watu binafsi.

Siku hiyo ndio tulishuhudia nchi yetu ikiwa katika ‘lockdown’ kwa karibu siku tano kwa baadhi ya maeneo ya nchi, lockdown ambayo ilitangazwa na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), na lockdown hiyo ikajirudi japo sio kwa ukali, Desemba 9, 2025.

Nitaanza na hili la maandamano, ni lazima tukubaliane kuwa nchi yetu inaongozwa kwa utawala wa sheria ambao ni lazima ukuu wa Katiba uonekane, wanaoongozwa watii sheria bila shuruti na watawala waheshimu Katiba na sheria.

Utawala wa sheria maana yake ni kwamba hakuna mtu aliye juu, au nje ya mamlaka ya sheria na hii ni kuanzia Rais wa nchi mpaka raia wa kawaida na kwa maneno mengine kila chombo cha Dola, taasisi au mtu anawajibika kwa sheria.

Iwe ni maandamano ya amani au sio ya amani, ni muhimu sana kujua ni wakati gani maandamano yanakuwa halali kisheria na ni wakati gani  yanakuwa haramu na kusababisha mvutano na vyombo vya dola nchini.

Bila kufahamu hili, tunaweza kujikuta tunaiingiza nchi na Watanzania katika machafuko hata kama wanaotaka kuandamana wana hoja kiasi gani, kwa sababu jambo lolote linalofanyika nje ya sheria linakosa uhalali wa kisheria.

Kwa Tanzania, Ibara ya 20(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, ambayo ni sheria mama, inayosema kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani.

Inatoa ruksa kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani, na kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au masilahi yake au mengine.

Tanzania, pia, imeridhia mkataba unaojulikana kama African Charter of Human and Peoples Rights wa 1981, ambao unasema kila mtu ana haki kukusanyika na watu wengine, lakini inaweza kuzuiwa na sheria kwa sababu za usalama wa Taifa.

Kwa Tanzania, sheria inataka waandaaji wa maandamano ya amani, watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi saa 48 kabla ya muda waliopanga kuandamana, na Polisi wana mamlaka ya kuyaruhusu au kuyazuia kwa sababu za kiusalama.

Ukisoma kifungu cha 11(4) cha Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019 kinasema pale ambapo maandamano yanaandaliwa na chama cha siasa, basi ni lazima waijulishe polisi saa 48 kabla ya maandamano ili watoe ulinzi.

Kifungu kidogo cha (5) cha kifungu hicho cha 11 kinasema taarifa ya kwenda polisi ni lazima ionyeshe muda na mahali maandamano yatafanyika na ajenda na baada ya kutoa taarifa wanaweza kuendelea, isipokuwa kama watapata zuio la polisi.

Sasa tuje kwenye hicho kilichoitwa maandamano ya Oktoba 29 na Desemba 9, yaliandaliwa na nani, taarifa imetolewa kwa mkuu gani wa kituo cha Polisi (OCS), nini ajenda ya maandamano, yangepita njia gani na je, polisi waliyapa baraka?.

Maandamano ya amani hujengwa juu ya msingi wa kisheria wa haki na wajibu.

Wakati Watanzania tuna haki ya maandamano, tunao wajibu mkubwa wa kutunza na kuheshimu sheria za nchi, moja ya sheria hiyo ni ile inayotutaka kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi si chini ya saa 48 tunapotaka kufanya maandamano.

Sasa, Oktoba 29 ilikuwa ni siku ya uchaguzi mkuu, ni siku muhimu sana ambayo hutokea kila baada ya miaka mitano. Ni siku ambayo Serikali na raia wanakuwa na taarifa nayo kwa miaka mitano kabla kwamba itakuja kutokea.

Ni siku ya alama ya kidemokrasia. Vyombo vya dola huwa vimejiandaa katika siku kama hiyo kwa ajili ya jambo moja kuu, kuhakikisha siku hiyo amani inatawala. Suala la ulinzi kwa siku hiyo huwa ni kipaumbele cha juu sana cha vyombo vyetu.

Vilevile, siku ya maadhimisho ya uhuru wa Tanganyika Desemba 9, unapangaje maandamano kama sio kutafuta ugomvi na vyombo vyetu vya dola?

Mtasema ooh, polisi tukiomba wanatukatalia kibali kwa sababu za kiintelijensia na ambazo hazina mashiko wala uhalisia, sawa. Kwani sheria si imeweka utaratibu wa rufaa? Waziri akikataa si kuna utaratibu wa maombi ya mapitio ya mahakama?.

Hivyo, tunavyopambania utawala wa sheria ni lazima na sisi tutembee kwenye msingi huohuo wa kuheshimu sheria na taratibu zetu kwa sababu dhambi ya kutoheshimu utawala wa sheria ni machafuko na kupotea kwa amani.

Nije kwenye uchambuzi wa faida na hasara za kiuchumi-kijamii zinazotokana na machafuko ya kiraia, maandamano haramu na lockdown hapa Tanzania ambapo wananchi wake wengi wanaishi kwa mkononi hadi kinywani au “hands to mouth”.

Kwa Tanzania, takwimu zinaonyesha zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wanaishi kwa mapato ya kila siku (kazi za mchana, wauzaji wadogo barabarani, wakulima wadogo, wafanyakazi wa kawaida) ambazo tunaziita hands to mouth.

Matukio ya Oktoba 29 na Desemba 9 yamejumuisha amri ya lockdown na vizuizi vya harakati wakati wa maandamano na hata mtandao wa intaneti kuzimwa na inakadiriwa kimataifa, kuzimwa intaneti kulisababisha hasara ya Sh560 bilioni.

Machafuko na maandamano husababisha biashara kufungwa, usafiri kusimama na masoko kuharibika na vurugu zile za Oktoba 29, zilifanya bei za chakula ziongezeke mara tano katika baadhi ya maeneo hasa Jiji la Dar es Salaam, Arusha na Mwanza.

Pia, watu wanaoishi mkono hadi kinywani,  hawana kinga dhidi ya mshtuko wa ghafla kwani vurugu zile ziliharibu miundombinu kama ya mwendokasi, majengo ya umma na binafsi kama vituo vya mafuta, ambao huathiri maisha ya kundi hili.

Lakini kuna athari za muda mrefu kwa uchumi hasa ikizingatiwa kuwa watalii na wawekezaji wa nje hukimbia kukuwa na machafuko.

Utalii unachangia karibu asilimia 17 ya pato la Taifa, na uharibifu wa picha ya nchi hupunguza fursa za watalii kuja nchini, biashara ya nje (korosho, dhahabu) inapata mtikisiko na wakulima wadogo nchini Tanzania ndio wanaumia zaidi na kadhia hii.

Lakini maandamano ya amani (sio haya tunayoyashuhudia ambayo hayafuati sheria) yanaweza kuwa na faida kwani yanaweza kulazimisha Serikali kurekebisha ufisadi, ukosefu wa haki, utekaji, watu kupotezwa, mauaji na ukosefu wa usawa.

Vurugu zile za Oktoba 29, 2025 zimevuta hisia za kimataifa, na yanaweza kusababisha uchaguzi wa haki zaidi na sera bora za kusaidia maskini.

Wakati mwingine machafuko yanawafanya watu wanaodai kunyanyaswa wawe na sauti kubwa zaidi, na kuunda umoja wa kudai haki kama ambavyo sasa tunaona vijana wa kizazi cha sasa maarufu kama Gen Z wakiunganisha nguvu kudai haki.

Lakini vurugu au machafuko makubwa yanaweza kuleta shinikizo la kimataifa kama ambavyo tayari tumeanza kuona kwa nchi za Jumuiya ya Ulaya (EU), na matishio ya kupungua misaada zaidi kwa miradi ya kupunguza umaskini, ikiwa Serikali itabadilika.

Katika Tanzania ambapo wengi wanaishi mkono hadi kinywa, hasara za machafuko ya kiraia, maandamano haramu na lockdown ni kubwa sana kuliko faida.

Ghasia za Oktoba 29, 2025 zilikuwa mbaya  zaidi na hatujawahi kuzishuhudia na hii inaonyesha namna ghasia zinavyoweza kuharibu maisha ya kila siku kwa haraka.

Maendeleo ya kweli yanahitaji kushughulikia mizizi ya matatizo ambayo kwa Tanzania kwa sasa ni hitaji la Katiba mpya, uchaguzi wa haki, kuheshimu utawala bora na kukomesha vitendo vya utekaji, kupotea kwa watu na mauaji ya kidola.

Lakini Jeshi letu la Polisi liepuke kukamata watu kiholela pasipo kufuata sheria jambo ambalo limeifanya iwe moja ya taasisi inayochukiwa zaidi na wananchi, lakini litekeleze majukumu yake kwa weledi na lisijiingize kwenye siasa.

Ni muhimu viongozi wakawa wasikivu na wakasoma alama za nyakati kwani ujasiri wa Gen Z wa Oktoba 29 umevunjwa ule wimbo tuliokuwa tunauimba na kuukariri kila siku kuwa “Watanzania hawawezi kuandamana”. Hiki ni kizazi kingine.

Tuache kushupaza shingo na tutoke hadharani na kukubali kuna mahali tumeteleza, tukiri tumeua raia ambao hata walikuwa hawaandamani, tuunde tume huru na inayoaminika kuchunguza na tuwawajibishe waliohusika.

Tukifikia hapo, naamini hata Gen Z wataweka silaha zao chini, kwa sababu ni mwendawazimu tu atapuuzia madai yao.

Maridhiano hayawezi kuja kabla ya watu kutubu kuna mahali walikosea na wala tusitumie propaganda kusingizia mabeberu au vita ya kiuchumi.

Mabeberu sio wanaokataa tusiwe na Katiba mpya, sio wanaoteka na kupoteza watu wala sio mabeberu wanaofanya chaguzi zetu zisiwe za huru na haki na wala si mabeberu wanaoelekeza polisi kukamata watu kiholela bila kufuata sheria. Tujitafakari.

Ndio maana nasema Tusishupaze shingo, kila aliyepotoka atubu kwa Mungu wake.

0656600900

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *