Shirika la habari la Reuters limezinukuu duru za kuaminika na kuripoti kuwa, serikali ya Marekani imewasiliana kwa siri na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC na kutishia kuiwekea vikwazo vipya ikiwa itajaribu kumshtaki Rais wa Marekani Donald Trump kwa uwezekano wa kuhusika na uhalifu.

Kwa mujibu wa Reuters, afisa mmoja wa serikali ya Washington amesema, wameitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, iifanyie marekebisho hati ya kuasisiwa kwake ili kuhakikisha kwamba hakuna uchunguzi wowote utakaofanywa dhidi ya Trump na maafisa wakuu katika serikali yake.

Shirika hilo la habari limeongeza kuwa, Ikulu ya White House ina wasiwasi wa kuja kutolewa uamuzi wa kumfuatilia kisheria Trump baada ya muhula wake wa urais kumalizika mwaka wa 2029, na kwa sababu hiyo, inataka ICC iufanyie mabadiliko Mkataba wa Roma ili kutoa kinga kwa viongozi wa Marekani.

Ripoti ya Reuters imebainisha kuwa, mashambulizi dhidi ya Iran, Somalia, Yemen na Carribean, pamoja na kutoa usaidizi wa silaha kwa utawala wa kizayuni wa Israel ni miongoni mwa kadhia zinazoweza kuzifanya nchi zimshtaki Trump kwa kutenda uhalifu wa kivita.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ina nchi wanachama 125, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Ulaya, lakini China, Russia na Marekani si wanachama wa mahaka hiyo.

Pamoja na hayo, mamlaka iliyonayo ICC ni pamoja na kuwashtaki watu binafsi, kama vile wakuu wa nchi, kwa uhalifu uliofanywa ndani ya ardhi ya nchi wanachama.

Itakumbukwa kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani Trump aliwawekea vikwazo baadhi ya maafisa wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kwa kutoa hati za kukamatwa viongozi wa utawala wa kizayuni wa Israel akiwemo waziri mkuu wake Benjamin Netayahu wanaotuhumiwa kufanya uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika vita vy Ghaza…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *