
Mkuu wa idara ya usalama wa kimtandao ya utawala wa kizayuni wa Israel (INCD) amesema, operesheni za kimtandao za Iran za wakati wa vita vya siku 12 mnamo mwezi Juni zilikuwa na wigo mpana kutosha kumfikia kila raia wa Israel na kwamba Tehran ilikuwa ikipanga na kufanya mashambulizi ya makombora dhidi ya maeneo yaliyolengwa kama vile Taasisi ya Weizmann kwa kudukua kwanza kamera za usalama za maeneo hayo.
Yossi Karadi ametoa kauli hiyo katika hotuba yake ya kwanza kwa umma tangu ashike wadhifa huo mnamo mwezi Machi na kueleza kwamba: “Iran ilijaribu kumfikia kila Muisraeli mara kadhaa, si mara moja, wakati wa vita vya siku 12 kwa kutumia silaha za kimtandao”.
Akihutubia katika mkutano wa wiki ya usalama wa kimtandao katika chuo kikuu cha Tel Aviv, Karadi amesema, Tehran iliendesha kampeni 1,200 tofauti za habari na taarifa ikiwa ni pamoja na jumbe za maandishi na machapisho ya mitandao ya kijamii wakati wa vita hivyo, kila moja ikiwalenga maelfu ya Waisraeli kwa wakati mmoja.
Afisa huyo wa Kizayuni amebainisha pia kwamba, wakati wa vita hivyo, Iran ilizihodhi kamera za maeneo ya maegesho na kamera za barabarani ili kufuatilia na kunasa nyendo za watu muhimu sana kwa lengo la kupanga operesheni za kuwalenga na kuwadhuru.
“Wakati Taasisi ya Weizmann ilipopigwa kombora, shambulio hilo halikuanzia hapo. Muda mfupi kabla, mshambuliaji alituma barua pepe za vitisho kwa wafanyakazi wa kituo hicho. Wakati huo huo, wakadhibiti kamera ya barabarani iliyokuwa ikisimamia jengo hilo lililoshambuliwa”, ameungama Karadi.
Ameongeza kuwa Iran ilituma pia barua pepe za vitisho kwa wafanyakazi katika idara mbalimbali za kituo hicho kabla ya shambulio hilo ili kuongeza athari za kisaikolojia.
Mkuu huyo wa idara ya usalama wa kimtandao ya utawala wa kizayuni amebainisha pia, kutolewa na Iran taarifa zilizovuja, ilikuwa hatua nyingine iliyochukuliwa na Tehran ili kuzidisha hofu…/