Shinyanga. Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amemtaka Meya wa Shinyanga, Salum Kitumbo na naibu wake, Pendo Sawa kutanguliza mbele maslahi ya wananchi kwani itasaidia kuleta maendeleo kwa amani na utulivu ndani ya mkoa huo.

Akizungumza leo Desemba 12, 2025 katika mkutano wa kuwatambua rasmi Meya na Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, iliyofanyika katika ofisi yake, amesisitiza umuhimu wa kuwa na maono mapana ya maendeleo

“Ni matumaini yangu kwamba mtatumia nafasi zenu kusimamia maendeleo ya kweli, viongozi tuwe mfano kwa kutanguliza maslahi ya wananchi ili kusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo kwa amani na utulivu.

“Pia, mkoa uko tayari kushirikiana nanyi kuhakikisha wananchi wa Shinyanga wananufaika na uongozi wenu,” amesema Mhita.

Kwa upande wake, Meya Kitumbo ameeleza kuwa hatua hiyo ya kujitambulisha ni mwanzo wa ushirikiano wenye tija kati ya Manispaa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ikiwa lengo ni kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati kwa tija na kwa manufaa ya wananchi wote.

“Kutambulika huku rasmi kutarahisisha ushirikiano kati ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Manispaa katika kuwatumikia wananchi, ni jambo la busara kufika mapema ili tuanze rasmi safari ya ushirikiano wa kweli kwa ajili ya maendeleo ya watu wetu,” amesema Kitumbo.

Naye Naibu Meya, Pendo Sawa amesema atafanya kazi bega kwa bega na meya katika kuhakikisha kila mwananchi anaguswa na huduma za maendeleo huku akisisitiza kuwa wapo tayari kupokea maelekezo ya kitaifa na kimkoa kwa ajili ya mafanikio ya manispaa.

“Tuko tayari kuwa mfano kwa kutanguliza maslahi ya wananchi na kuhakikisha kila mwananchi anaguswa na huduma za jamii na kunufaika na maendeleo ya manispaa, pia tuko tayari kwa maagizo yoyote kwa ajili ya mafanikio ya manispaa,” amesema Pendo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *