BAADA ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa Oktoba 29, 2025 kupita, serikali imesisitiza kuwa inachukua hatua ya maridhiano kuhakikisha mazungumzo kati yake na makundi mbalimbali ili kujenga taifa lenye amani na umoja.

Akizungumza mwanzoni mwa mwezi Novemba, mwaka huu, Makamu wa Rais Dk Emmanuel Nchimbi anasema ni dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha serikali inaanzisha mazungumzo ya maridhiano ili kuhakikisha watu hata wanapata nafasi ya kusikilizwa.

Anasema uamuzi huo wa Rais Samia unalenga kuwa na taifa lenye amani na umoja na kuendelea kuwa mfano wa utulivu katika Afrika na dunia nzima. Kwa kutambua umuhimu wa dhamira hiyo ya serikali, wanawake nao wanaunga mkono suala la mazungumzo kwa ajili ya kuzidi kuimarisha amani na mshikamano nchini. SOMA: Wanawake waja na maazimio 5 kuimarisha amani

Akiwa katika Jukwaa la Wanawake 2025 lililofanyika Dodoma hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Asha-Rose Migiro anasema wanawake ni nguvu ya taifa. Kwa msingi huo anasema wanawake na Watanzania wote kwa ujumla, wana mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa lao ikiwa ni pamoja na kukaa pamoja na kujadili changamoto zinazotokea.

Hizi ni pamoja na changamoto za kijamii, kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni, kiteknolojia na changamoto za amani nchini. Dk Migiro anasema Watanzania hawana sehemu nyingine ya kwenda isipokuwa Tanzania hivyo ni muhimu kutorudia yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, mwaka huu na kuyumbisha amani ya taifa.

“Tumeona jinsi serikali ilivyosimama imara kuhakikisha kwamba utulivu unarejea na kuhakikisha shughuli za uzalishaji zinaanza tena,” anasema. “Hii inakwenda sambamba na ile Falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya mambo makubwa manne ambapo mojawapo ni ustahimilivu,” anasema. Mwanasiasa huyo anasema Watanzania wana wajibu wa kuhakikisha taifa linakuwa salama, imara na kuweka mazingira mazuri ya kusonga mbele.

“Tumeona nafasi ya maridhiano, nafasi ya mazungumzo, huu ni wakati wetu sisi kuitikia wito huu, tuwe ni sehemu ya mazungumzo,” anasisitiza. Anasema pamoja na uwepo wa tume inayochunguza kiini cha vurugu hizo, Watanzania pia wana wajibu wa kuendelea kuweka mazingira mazuri ili washiriki katika mchakato muhimu wa safari ya maridhiano na kuimarisha maridhiano yaliyopo.

“Kilichotokea (vurugu za Oktoba 29, 2025) si utamaduni wetu Watanzania, si hulka yetu na wala si maisha ambayo Watanzania tumekuwa tukiishi yaliyotupatia sifa kubwa duniani ya Tanzania kuwa kisiwa cha amani na utulivu,” anasema.

Anaongeza: “Tufanye kila liwezekanalo kurejea tena katika nafasi yetu na kuifanya Tanzania iendelee kuwa nchi kiongozi katika suala la amani, utulivu na maendeleo.” Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Taifa, Mary Chatanda anasema jukwaa hilo limeazimia kuwa wanawake wataendeleza misingi ya upendo heshima, mazungumzo ya kuvumiliana na utatuzi wa migogoro mambo ambayo ndiyo msingi wa amani ya Tanzania.

“Kama wazazi na walezi, wanawake tunatambua wajibu wetu wa kuendeleza misingi ya upendo, heshima, mazungumzo ya kuvumiliana na utatuzi wa migogoro, huu ndio msingi wa amani ya Tanzania,” anasema Chatanda. Anasema wamejizatiti kuanzisha na kuhimiza majukwaa ya mazungumzo ya amani kwenye familia, mitaa na makundi mbalimbali ikiwa ni njia pekee ya kuimarisha mshikamano na kuondoa tofauti zinazoleta migawanyiko.

“Tumeazimia kuwa mabalozi wa maudhui yanayojenga umoja, kuheshimiana, kutunzana na kulinda hadhi ya taifa, tunapinga taarifa potofu, lugha za chuki na kauli zinazoleta mpasuko katika jamii,” anasisitiza. Anasema wanawake wameazimia kuwa mstari wa mbele kutambua viashiria vya migogoro katika jamii na kutumia hekima, ushawishi na umoja wetu kuhimiza uvumilivu, utulivu, maelewano na mazungumzo yanayojenga.

“Hatua hizi ndizo mwendelezo wa safari yetu ya pamoja ya kujenga jamii yenye amani, utulivu, matumaini na fursa kwa wote,” anasema. Katika kongamano hilo, Balozi Christopher Liundi anahimiza wanawake, vijana na Watanzania wote kufanya kazi na kuzungumza ili kupata tabasamu na kuliwezesha taifa kusonga mbele.

Anasisitiza umuhimu wa watu kuzungumza ili kupata mwafaka zinapotokea changamoto. Balozi Liundi anasisitiza tabasamu kuwa dawa, njia na utaratibu utakaofikisha taifa mbali kimaendeleo. Anawataka wanawake hao kuendelea kuwa na moyo wa kukaa pamoja na kushirikiana kwani wameonesha mfano mzuri wa kuona umuhimu wa kuitana pamoja na kuzungumzia suala la amani nchini.

“Ombi langu kwenu nyote na sisi wote ni kwamba, tushikamane tuwe pamoja, tuungane katika shughuli zetu huku tukiyaona mema kwa sababu kuzungumza na kutabasamu kunatoa nafasi ya kutoa hewa na kuitoa nje na kuingiza nyingine safi,” anasema Liundi.

Mchumi na Mwanamke wa Kwanza kuwa Mwekahazina wa CCM-Taifa, Sifa Swai anasema ulinzi wa amani hauishii barabarani na nyumbani pekee, bali huendelea hadi kwenye mitandao ya kijamii ambayo wakati mwingine imekuwa ikitumika vibaya kama jukwaa la kusambaza habari potofu.

“Tanzania ya tabasamu inahitaji kila mmoja wetu kushiriki katika kutunza na kulinda amani ya nchi na ustawi katika ngazi zote kuanzia ngazi ya familia hadi taifa,” anasema. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dk Tatu Nyange anasema amani hudumu pale ambapo mwanamke anapewa nafasi ya kuongoza na kufanya uamuzi. Anaongeza kuwa kuna umuhimu wa kuwekeza kwa makusudi katika nafasi ya wanawake kama walinzi wa amani, maadili na maridhiano ya kweli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *