Wajumbe waliotumwa na Rais Donald Trump kwenye mazungumzo hayo ya Berlin, Ujerumani, walimpa fursa hiyo Rais Volodymyr Zelensky, lakini walionya kwamba pendekezo hilo lisingelibakia muda mrefu ikiwa halikukubalika sasa.
Jijini Washington, Trump aliwaambia waandishi wa habari kwamba utawala wake unajaribu kuhakikisha makubaliano yanapatikana.
Rais huyo wa Marekani aliongeza, akiwa Ikulu ya White House baada ya kuzungumza na wawakilishi wake mjini Berlin kwamba: “Tumekuwa na duru kadhaa za mazungumzo na Rais Vladimir Putin wa Urusi na nadhani tupo karibu zaidi kufikia makubaliano kuliko tulivyowahi kuwa hapo kabla. Ngoja tuone kitakachotokea.”
Zelensky alisema baada ya mazungumzo hayo kwamba angeliiomba Marekani kuiwekea vikwazo vipya Urusi na kuipatia nchi yake silaha zaidi, “ikiwa Moscow itakataa mapendekezo yanayojadiliwa kati ya Kiev, Washington na viongozi wa Ulaya,” lakini hakusema ikiwa amekubali moja kwa moja pendekezo la kuiachia mikoa miwili ya Donestk na Luhansk kama unavyotaka utawala wa Trump.
Viongozi wa Ulaya wapokea kwa hadhari
Mazungumzo hayo ya jioni ya Jumatatu (Disemba 15) katika mji mkuu huo wa Ujerumani yalizusha matumaini mapya kwa viongozi wa Ulaya juu ya kupatikana njia ya kukomesha mgogoro huo mbaya kabisa kwenye ardhi ya Ulaya tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia.
Hata hivyo, wengi wao walilipokea pendekezo la utawala wa Trump juu ya hakikisho la usalama kwa Ukraine kwa tahadhari.
Licha ya kuusifia ushirikiano mkubwa wa Trump, Zelensky na Ulaya uliofanikisha hatua hiyo ya sasa, Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen, alisema “suala la mamlaka ya Ukraine linapaswa kuamuliwa tu na Waukraine wenyewe.”
“Mahakikisho haya ya kiusalama lazima yazingatiwe kwa misingi iliyo imara. Tutaheshimu uamuzi unaofanywa na Ukraine yenyewe. Maamuzi kuhusu mamlaka ni lazima yachukuliwe na Ukraine na Ukraine pekee. Vivyo hivyo, masuala yanayougusa Umoja wa Ulaya na NATO yatajadiliwa na wajumbe wa Umoja wa Ulaya na NATO. Kwa ufupi, hakuna lolote kuhusu Ukraine bila Ukraine, lolote kuhusu Ulaya bila Ulaya na lolote kuhusu NATO bila NATO.” Alisema von der Leyen.
Kauli kama hiyo zimetolewa pia na Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani, Waziri Mkuu wa Poland, Donald Tusk, na Waziri Mkuu wa Sweden, Ulf Kristersson, ambao wote walionesha uungaji mkono wao kwa hakikisho la usalama la Marekani kwa Ukraine, lakini wakati huo huo wakiashiria kuwa uamuzi wa mwisho ni wa Kiev na wakitilia shaka endapo Moscow ingelikubaliana nao.
Bado Urusi haijasema ikiwa imekubaliana na mabadiliko yoyote yaliyofanyika kwenye pendekezo la Trump, na haijaonesha dalili ya kutoa uamuzi huo kwa sasa.