Mapinduzi mara mbili na jaribio moja lililoshindikana katika kipindi cha wiki nane, mwelekeo huu wa hivi karibuni ni mpya katika historia ya bara la Afrika. Mnamo Oktoba, jeshi nchini Madagascar lilimwondoa Rais wan chi hiyo baada ya wiki kadhaa za maandamano na mnamo mwezi Novemba, wanajeshi nchini Guinea-Bissau walimwondoa mkuu wa nchi muda mfupi baada ya kile walichokiona kuwa uchaguzi uliokuwa na udanganyifu.
Vilevile mwanzoni mwa mwezi Desemba, kundi la wanajeshi, wanaojiita “Kamati ya Kijeshi ya Urekebishaji,” walitangaza kuchukua madaraka nchini Benin, lakini hawakufanikiwa na hatimaye walikamatwa baada ya walinzi wa rais na washirika wa kikanda kuingilia kati.
Kwa sasa, nchi nane barani Afrika zinatawaliwa kijeshi, ukanda huu wa mapinduzi unaenea kote barani humo, Pamoja na eneo la Sahel, hasa katika nchi zinazozungumza lugha ya Kifaransa. Je ni kwa nini kuna matukio mengi ya mapinduzi mengi barani Afrika kwa sasa na je, mabadiliko haya yanatishia kuingia kwenye nchi zingine za bara hilo pia?
Huko mjini Dakar, Senegal, Beverly Ochieng, mtafiti katika mpango wa Afrika kwenye Kituo cha Masomo ya Kimkakati na Kimataifa (CSIS) chenye makao yake makuu nchini Marekani amesema:
“Ni vyema kuangalia vichocheo hivi vyote kama. Je, kuna kiwango cha juu cha malalamiko ya kiuchumi na kijamii? Je, kuna mashaka ndani ya jeshi kuhusu wayotendewa au kama wanajeshi wanalipwa mshahara wa kutosha au mazingira yao ya kazi ni sahihi? Inafaa pia kuangalia iwapo kuna wachochezi wa nje ambao wanataka kutumia fursa ya kutoridhika na serikali katika nchi husika na kisha kujaribu kuhamasisha watu kwa kiwango kikubwa na kujaribu kuvuruga mshikamano wa taasisi zake? Haya ni baadhi tu ya mambo ambayo yanafaa kuangaliwa.”
Bibi Ochieng amebainisha hatari ya mapinduzi mapya katika nchi za Sahel za Mali, Burkina Faso, na Niger, ambazo tayari ziko chini ya utawala wa kijeshi. Amesema Chad pia inapaswa kufuatiliwa kwa karibu, kwani kuna kutokukubaliana ndani ya jeshi lake.
Vichocheo Vitatu vya Mapinduzi
Naye mwanzilishi na mwenyekiti wa bodi ya Taasisi ya Mafunzo ya Usalama ya Afrika Kusini (ISS ) Jakkie Cilliers, amesisitiza alipozungumza na DW kwamba Afrika haina tofauti na mabara mengine, amesema nchi nyingi za Afrika zinakabiliwa na changamoto maalum: kwa mfano “Katika Afrika Magharibi na eneo la Sahel, amesema baadhi ya nchi zinakabiliwa na ukuaji wa haraka sana wa idadi ya watu na kwamba vijana wengi, hasa wa kiume, ndio mara nyingi huwajibika kwa ukosefu wa utulivu, wengi wao ni wale waliopata elimu bora lakini hawana kazi na hakuna fursa. Cilliers amesema hii ni hali tete inayoweza kusababisha ukosefu wa utulivu.
Anailinganisha hali hiyo ya kijamii na kiuchumi na petroli inayolowesha kitambaa kwa kusema kadiri petroli inavyozidi kuwa nyingi, ndivyo cheche nazo zinavyozidi kuwa hatari.
Mwanzilishi na mwenyekiti wa bodi ya Taasisi ya Mafunzo ya Usalama ya Afrika Kusini (ISS ) Jakkie Cilliers, amesema mapinduzi yaliyotokea katika miaka ya hivi karibuni, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, na Umoja wa Afrika (AU) zimechukua hatua katika kuzisimamisha uanachama na kuziwekea vikwazo nchi zenye kufanya mapinduzi lakini amesema hana uhakika kama hatua kama hii itakuwa na athari ya kuzuia mapinduzi na ameongeza kusema kuwa matatizo haya yamejikita sana, ni ya kimuundo, na hakuna suluhisho la muda mfupi la kutatua matatizo hayo barani Afrika.
Jakkie Cilliers, amesema hii pia ina maana kwamba hatari ya mapinduzi inaweza tu kupunguzwa kupitia maendeleo mazuri ya muda mrefu ambapo wananchi wote wa nchi husika watashirikishwa kiuchumi kielimu, na pia upatikanaji wa mahitaji ya msingi na haki.