
Hadi sasa baadhi ya familia zinasubiri kusikia kuhusu hatma ya ndugu na jamaa zao ambao hadi sasa hawajulikani waliko huku mamlaka za serikali zikilaumiwa kwa mara nyingine kwa kuruhusu boti kusafiri bila kuzingatia kanuni madhubuti za usalama.
Familia zinaomboleza vifo vya wapendwa wao na nyingine zinahangaika kuwatafuta wale waliopotea kwenye ajali hiyo ya boti iliyotokea Jumamosi iliyopita katika kijiji cha Bolo, ndani ya eneo la Bagata, Mkoa wa Kwilu.
Wengine wangali wamejaa kwenye mwambao mwa mto kongo kuwasubiri taarifa za wapendwa wao. Dally Kimpana ni mmoja wa manusura na hapa anaeleza masaibu yaliompata. “Tulikuwa katika boti hiyi usiku.nikasikia kitu kinatoa sauti kubwa kubwa, na nikaanza kuona boti inaelemewa kwa maji.Tulikuwa wengi katika boti hiyo zaidi ya watu mia moja pamoja na mizigo. Waliookolewa ni chini ya watu 50. Rafiki yangu ambaye ni mwalimu na mtoto wake walifariki.Mimi nilipona sababu nilishikilia mfuko wa mkaa uliokuwa karibu yangu. Tatizo tulisafiri bila hata boya la kujiokoa.”
Hadi sasa, hakuna tangazo lililotolewa na mamlaka ya usafiri wa maji hapa nchini, lakini Garry Kasata ambaye ni mbunge wa eneo hilo anasema hapa idadi ya waliofariki na kwamba utafutaji unaendelea. “Kwasasa idadi ya waliofariki inafikia watu 30 na utafutaji unaendelea. Vitu Vingi vimepotea ikiwemo mizigo yote ya abiria, zaidi ya magunia 700 ya mahindi pamoja na mkaa. Wengi ya wasafiri walikuwa walimu waliokuwa wakienda kuchukuwa mishara yao huku BANDUNDU na wengine kwenda kusherehekea na familia zao.”
Wanaharakati wa kutetea haki za kinibadamu hapa nchini wameitiaka serekali ya DRC kufanya uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika wa mkasa huo.
Tangu mwezi Januari, zaidi ya watu 1,200 wamekufa kwenye njia za maji hapa nchini Kongo. Mwezi Septemba zaidi ya watu 146 walipoteza maisha katika ajali ya boti kwenye Mto Kongo, huku wengine 70 wakifariki kwenye mto Kasai. Serekali ya Kongo inanyooshewa kidole cha lawama kwa kushindwa kuchukuwa hatua madhubuti kusimamia safari za majini hapa nchini. Boti au meli zinazotumika ni chakavu, nyingine hazifanyiwi matengenezo huku nyingi zikibeba watu na mizigo kupita uwezo wake na hazina vifaa vya usalama na uokoaji.