Nairobi. Kampuni ya Kitanzania, Amsons Group, imesaini mkataba wa Dola250 milioni za Marekani (zaidi ya Sh600 bilioni ya Kitanzania) kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha klinka eneo la Matuga, Kaunti ya Kwale, Kenya.

Hatua hiyo inatajwa kuwa miongoni mwa uwekezaji mkubwa zaidi wa viwanda unaofanywa na Kampuni ya Tanzania nchini humo.

Mradi huo unafuatia ununuzi wa Bamburi Cement na Amsons Group na ni sehemu ya mkakati wa upanuzi wa kikanda unaolenga soko linalokua la ujenzi na miundombinu katika Afrika Mashariki.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba huo iliyofanyika jijini Nairobi jana na kushuhudiwa na Rais wa Kenya, William Ruto, Mwenyekiti wa Amsons Group, Edha Nahdi alisema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya muda mrefu ya kampuni hiyo katika kuendeleza viwanda katika ukanda

“Uwekezaji wa Dola 250 milioni unalenga moja kwa moja kupunguza utegemezi wa uagizaji wa klinka kutoka nje, huku ukiimarisha uwezo wa uzalishaji wa ndani kulingana na vipaumbele vya Serikali ya Kenya,” alisema Nahdi.

Kiwanda hicho kitajengwa kupitia kampuni tanzu ya Amsons, Bamburi Cement Plc na kinatarajiwa kuongeza uzalishaji wa klinka nchini humo, ambayo ni malighafi muhimu katika utengenezaji wa saruji.

Mtendaji Mkuu wa Bamburi Cement, Mohit Kapoor alisema mradi huo utaendana na mkakati wa kampuni wa uzalishaji wa saruji yenye kiwango cha chini cha uzalishaji wa hewa ukaa.

“Kiwanda cha Klinka cha Matuga kitawekwa teknolojia za kisasa zitakazopunguza uzalishaji wa hewa chafu na kuongeza ufanisi wa uzalishaji,” alisema.

Baada ya kuanza kazi, kiwanda hicho kinatarajiwa kupunguza utegemezi wa Kenya kwa klinka kutoka nje na kuimarisha uthabiti wa mnyororo wa thamani wa saruji katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mradi huo pia unatarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira 10,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, na kuchochea shughuli za kiuchumi katika eneo la Pwani.

Amsons Group, yenye makao yake makuu nchini Tanzania, imeendelea kupanua uwepo wake katika sekta ya saruji kikanda kufuatia ununuzi wa Bamburi Cement mwishoni mwa mwaka 2024 na kupata umiliki wa hisa nyingi katika Kampuni ya Saruji ya East African Portland Cement Company (EAPCC).

Kwa kushirikiana na uwekezaji mwingine unaoongozwa na Amsons, Kiwanda cha Matuga kinatarajiwa kuongeza uwezo wa uzalishaji wa klinka nchini Kenya hadi kuzidi mahitaji ya ndani.

Rais Ruto alisema sekta ya saruji ni mhimili muhimu wa utekelezaji wa miradi ya miundombinu, ikiwamo nyumba za gharama nafuu, usafirishaji, nishati na viwanda.

“Miradi kama Kiwanda cha Klinka cha Bamburi inaimarisha mnyororo wa thamani wa saruji na kusaidia ushindani wa muda mrefu, si kwa Kenya pekee bali kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki,” alisema.

Mkataba wa ujenzi wa kiwanda hicho ulisainiwa na Kampuni ya Sinoma–CBMI Construction Co Ltd, inayojishughulisha na uhandisi na ujenzi wa viwanda vya saruji.

Amsons Group ilisema uwekezaji huo unaakisi mchango unaoongezeka wa mtaji wa Kitanzania katika maendeleo ya viwanda, biashara ya mipakani na minyororo ya thamani katika Afrika Mashariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *