Katika kikao hicho ambacho kitagubikwa na mzozo wa mashariki ya Kati kufuatia hali mbaya ya kibinaadamu inayoshuhudia Gaza, mataifa kama Ufaransa, Canada, Australia, Uhispania, Norway, Ubelgiji na mengineyo yanatarajia kuitambua Palestina kama taifa huru ili kusisitiza umuhimu wa suluhisho la mataifa mawili.
Hata hivyo hatua hiyo ya kulitambua taifa la Palestina inapingwa vikali na Israel na mshirika wake mkuu Marekani.
Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ambaye ndiye rais mpya wa Mkutano huo wa 80 wa Baraza hilo lenye nchi wanachama 193 amesema katika hotuba yake ya ufunguzi kuwa ulimwengu unakabiliwa na mizozo mbalimbali na kwamba Umoja wa Mataifa bado unahitajika.
“Huu ni mwaka wa kubadilika, kupiga hatua na kujenga taasisi ya Umoja wa Mataifa tunayoihitaji kwa miaka 80 ijayo, kwa ajili ya maisha ya watoto wetu. Ni wakati wa kuwathibitishia watu bilioni nane duniani kote kwamba shirika hili bado ni muhimu, na kwa nini wanatakiwa kuamini kuwa bendera ya bluu inayopepea ya Umoja wa Mataifa ni chanzo cha matumaini.”
Baerbock ameendelea kusisitiza umuhimu wa Umoja wa Mataifa katika migogoro ya kimataifa kama masaibu ya wasichana wa Afghanistan kunyimwa elimu, watoto kufa njaa huko Gaza, na wakazi wa visiwa vya Pasifiki kuwa hatarini kutokana na kina cha bahari kuongezeka.
Hotuba ya Guterres kuhusu amani
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwekeza katika suala la kupambana na umaskini badala ya kuwekeza kwenye vita kunaweza kuifanya dunia kuwa salama zaidi huku akisisitiza umuhimu wa umoja na kuaminiana baina ya nchi ili kusonga mbele.
“Mkataba hauwezi kujitekeleza wenyewe. Kwa namna ulivyobuniwa, unahitaji nchi kutozingatia zaidi maslahi yao ya kitaifa na kuweza kujenga upya mazoea ya kuaminiana kati yao, na pia kuamini katika kile tunachoweza kutimiza kupitia ushirikiano na mshikamano.”
Katika kikao hicho cha 80 Cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mizozo mingine kama uvamizi wa Urusi nchini Ukraine au hata vurugu za miongo kadhaa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inatarajiwa kuibuliwa.
Vyanzo: DPA, Reuters, AP