Wadau waeleza matarajio tume ya uchunguziWadau waeleza matarajio tume ya uchunguzi

WADAU wa siasa na diplomasia wameeleza matarajio na imani yao kwa Tume Huru ya Uchunguzi ya vurugu zilizotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.

Wakiunga mkono uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuunda tume hiyo inayoendelea na kazi yake ikitajwa kuwa na wajumbe wenye weledi, miongoni mwa waliozungumza na HabariLEO jana, walisema ni jambo jema kwa kuwa matatizo ya Watanzania yatatatuliwa na Watanzania wenyewe.

Mwenyekiti wa Chama cha Ada Tadea, Juma Ali Khatibu, alisisitiza kuunga mkono uundwaji wa tume hiyo ambayo ilianza kufanya kazi Novemba 20, mwaka huu.

“Tanzania tunajuana wenyewe, haiwezekani kila jambo tukaita watu wa nje. Ada Tadea tuna imani na wajumbe walioteuliwa. Ushauri wetu tuache mtazamo wa ubepari na ubeberu, tupende vya kwetu na kuwatukuza wataalamu wetu,” alisema Khatibu.

Katibu Mkuu wa Chama cha NLD, Hassan Doyo amesema  haiwezekani jambo lifanyike ndani ya nchi kisha waitwe watu au wataalamu wa nje kuja kufanya uchunguzi. Amewataka wananchi kujenga tabia ya kuamini wataalamu wao. “Kwanza, nani mwenye mamlaka ya kuunda tume kwenye nchi ya watu? Nina imani na walioteuliwa, watatekeleza wajibu wao kwa haki.

Wale wote wenye ushahidi wajitokeze kwa uhuru mbele ya tume au watumie njia zilizotajwa za kutoa ushahidi wao,” alisema Doyo. Mwanadiplomasia, Balozi Dk Benson Bana amesema Rais Samia ana mamlaka ya kikatiba ya kuunda tume, huku akisisitiza kuwa wadau wana haki ya kutoa maoni, lakini ni lazima waheshimu mipaka ya mamlaka ya Rais.

“Tuiache hii tume ifanye kazi itekeleze wajibu wake kwa misingi ya haki, ukweli na uwajibikaji na wazingatie mwongozo waliopewa,” alisema Balozi Dk Bana. SOMA: Tume yafanya mahojiano RC Chalamila

Umahiri wa Tume Tume hiyo iliundwa Novemba 18, 2025 na Rais Samia. Mwenyekiti wake ni Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman, Balozi Ombeni Sefue, ambaye ni Mwanadiplomasia na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu. Jaji Chande ni kiongozi mwenye uzoefu katika tasnia ya sheria, utoaji wa haki na masuala ya haki za binadamu kitaifa na kimataifa.

Anafahamika na kuheshimika kimataifa kutokana na uelewa alio nao wa masuala ya sheria na siasa za kimataifa kwenye masuala ya utunzaji wa amani. Wajumbe ni Jaji Mkuu mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Ibrahim Juma aliyekuwa Jaji Mkuu tangu 2017, hadi alipostaafu mwaka huu.

Mjumbe mwingine ni Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue ambaye aliwahi pia kuwa Katibu wa Baraza la Mawaziri, Katibu wa Baraza la Usalama la Taifa na Mkuu wa Utumishi wa Umma. Mwingine ni mwanadiplomasia na Balozi mstaafu, Radhia Msuya ambaye alihudumu katika nchi mbalimbali akiwa balozi, ikiwemo Afrika Kusini, Namibia, Lesotho, Botswana na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Kutokana na weledi wake kazini, Balozi Msuya aliwahi kutunukiwa Nishani ya Heshima ya National Oder of Merit na Rais wa Ufaransa. Mwanadiplomasia na Balozi mstaafu, Paul Meela ambaye ni Luteni Jenerali mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), pia ni mjumbe na aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Akiwa kazini, Balozi Meela alishiriki katika shughuli nyingi za kuleta amani Darfur, Sudan na alishiriki katika usuluhishi katika timu ya usuluhishi chini ya Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta. Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IJP) mstaafu, Said Mwema pia ni mjumbe wa tume hiyo ambaye katika utumishi wake alifanikisha mageuzi makubwa ndani ya Jeshi la Polisi.

Amefanikiwa kuandaa na kutekeleza mkakati wa polisi jamii na kuliongoza jeshi la polisi kupambana na uhalifu, ukiwemo wa kuvuka mipaka, ugaidi, biashara haramu ya binadamu na dawa za kulevya. Wajumbe wengine ni mwanadiplomasia na Balozi mstaafu, David Kapya ambaye aliwahi kufanya kazi mbalimbali katika utatuzi wa migogoro, ikiwemo kuwa Msaidizi Mahususi wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa katika mazungumzo ya kutafuta amani Mashariki mwa DRC.

Mwingine ni aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dk Stergomena Tax ambaye ni kiongozi mwandamizi mstaafu mwenye uzoefu katika masuala ya uongozi, diplomasia na utangamano wa kikanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *