Dar es Salaam. Ni mambo ya bata batani! Wazungu husema ‘December to remember’ wakimaanisha ni mwezi wa kujenga kumbukumbu, kukutana na ndugu, jamaa na marafiki, na kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka.
Kwa wengi, sikukuu ni muda wa ‘kula bata’ bila mipaka kuanzia sherehe za ofisini, matamasha ya muziki, hafla za marafiki hadi mikusanyiko ya kifamilia inayochukua hadi usiku wa manane. Barabara hujaa magari, mitaa ya burudani huwa hai zaidi, na maisha ya usiku hufikia kilele chake. Ni katika muktadha huu ambapo mjadala wa namna ya kufurahia bila kuvuka mipaka ya usalama huibuka.
Kwa kawaida, mwezi wa Desemba huambatana na ongezeko la safari za usiku na matumizi ya pombe, hali inayofanya sherehe ziwe tamu zaidi lakini pia kuhitaji umakini zaidi katika maamuzi yanayofanywa mwishoni mwa usiku. Wengi hupenda sherehe ziishe kwa furaha ileile zilivyoanza kila mmoja akirejea nyumbani salama tayari kuendelea na shamrashamra za siku inayofuata.
Ndani ya mazingira hayo ya sikukuu, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kwa kushirikiana na Bolt wamekuja na kampeni iitwayo ‘Wrong Side of the Road (WSOTR)’ ikilenga kuwahamasisha Watanzania kufanya maamuzi sahihi na salama, baada ya kusherehekea na kupunguza ajali zinazotokana na kuendesha gari ukiwa wamelewa.
Moja ya vivutio vya kampeni hii ni motisha kwa wanaosherehekea, ikiwemo punguzo la usafiri kupitia Sherehe Code kwa wanaoshiriki mafunzo mafupi ya uelimishaji.
Aidha, baadhi ya wasafiri hupata bahati ya kupanda Special Bolt gari lenye mvuto wa sikukuu, muziki na mandhari inayoongeza ladha ya sherehe hata safari ya kurudi nyumbani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Meneja Mawasiliano na Uendelevu wa SBL, Rispa Hatibu, amesema sikukuu ni sehemu ya utamaduni wa Watanzania na hakuna sababu ya kuzizuia.
“Tunataka watu wafurahie, wacheke, washerehekee na kula bata. Lakini furaha ya kweli ni ile inayomruhusu mtu aamke kesho yake akiwa salama na tayari kuendelea na maisha,” amesema.
Msimu huu wa sikukuu pia unaonesha mabadiliko ya mtazamo kwa vijana na jamii kwa ujumla, ambapo sherehe zinaanza kuhusishwa zaidi na uzoefu mzima furaha, muziki, marafiki na usalama badala ya pombe pekee. Ni sikukuu inayohimiza raha yenye mipaka, burudani yenye heshima kwa maisha.
Mkuu wa Bolt kwa Tanzania, Kenya na Uganda, Dimmy Kanyankole, amesema ushirikiano huo unalenga kurahisisha upatikanaji wa usafiri salama katika kipindi chenye msongamano mkubwa wa safari.
“Msimu wa sikukuu ni miongoni mwa vipindi vyenye shughuli nyingi zaidi, watu husafiri zaidi, hukaa nje kwa muda mrefu na kufanya maamuzi ya ghafla. Lengo letu ni kuondoa vikwazo vya usafiri salama kwa kuufanya uwe rahisi, nafuu na unaopatikana pale unapohitajika zaidi,” amesema Kanyankole.
Kampeni hii itaendeshwa katika kipindi chote cha sikukuu, ikianza na shughuli katika maeneo makubwa ya burudani na maisha ya usiku jijini Dar es Salaam, kabla ya kupanuliwa kwenda mikoa mingine nchini.