Hata hivyo, hali bado ni tete, huku zaidi ya robo tatu ya wakazi wakikabiliwa na njaa kali na utapiamlo, kwa mujibu wa tathmini mpya iliyotolewa leo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya IPC ambao ni mfumo wa kimataifa wa kufuatilia utapiamlo na ukosefu wa uhakika wa chakula, hakuna maeneo ya Gaza kwa sasa yaliyoainishwa kuwa katika hali ya njaa daraja la 5 la IPC, kufuatia kuimarika kwa upatikanaji wa misaada ya kibinadamu na biashara baada ya usitishaji mapigano wa tarehe 10 Oktoba.
Hata hivyo, karibu Ukanda mzima wa Gaza bado uko katika hali ya dharura kutokuwa na uhakika wa chakula daraja la 4, huku mamia ya maelfu ya watu wakiendelea kukumbwa na viwango vya juu sana vya utapiamlo mkali.
Katikati ya Oktoba na mwishoni mwa Novemba, takribani watu milioni 1.6 sawa na asilimia 77 ya idadi ya watu waliotathminiwa walikabiliwa na njaa ya kiwango cha mgogoro daraja la 3 au mbaya zaidi.
Kati yao, zaidi ya watu 500,000 walikuwa katika hali ya dharura ya darala la 4 na zaidi ya 100,000 walikuwa katika hali ya janga la daraja la 5, ripoti imesema.
Familia iliyofurshwa na vita imesimama nje ya hema lao la muda katika Jiji la Gaza.
Mafanikio dhaifu kwa hatari kubwa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema matokeo ya hivi karibuni yanaonesha maendeleo, lakini akaonya kuwa mafanikio hayo bado ni “dhaifu na kwa hatari kubwa.”
Guterres amewaambia waandshi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York “Njaa kali imesogezwa nyuma. Watu wengi zaidi sasa wanaweza kupata chakula wanachohitaji ili kuendelea kuishi.”
Hata hivyo, ameongeza kuwa watu milioni 1.6 huko Gaza zaidi ya asilimia 75 ya wakazi “wanatarajiwa kukabiliwa na viwango vya juu sana vya ukosefu wa uhakika wa chakula wa ghafla na hatari kubwa za utapiamlo.”
Tathmini ya IPC inakadiria kuwa hadi katikati ya Aprili 2026, takribani watu 571,000 wataendelea kuwa katika hali ya dharura, huku karibu watu 1,900 wakitarajiwa kuendelea kukabiliwa na njaa ya kiwango cha janga.
Katika hali mbaya zaidi ikiwemo kurejea kwa mapigano au kusitishwa kwa uingiaji wa misaada ya kibinadamu na biashara Ukanda mzima wa Gaza unaweza tena kukabiliwa na njaa kali.
Utapiamlo wasalia kuwa tatizo kubwa
Utapiamlo bado ni tatizo kubwa, hususan miongoni mwa watoto na wanawake wajawazito na wanaonyonyesha.
Takribani watoto 101,000 wenye umri wa miezi sita hadi 59 wanatarajiwa kukumbwa na utapiamlo mkali hadi katikati ya Oktoba 2026, wakiwemo zaidi ya 31,000 walio katika hali mbaya zaidi. Inakadiriwa pia kuwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wapatao 37,000 watahitaji matibabu.
Ingawa misaada ya chakula imeongezeka, ripoti inasisitiza kuwa msaada huo kwa kiasi kikubwa unakidhi mahitaji ya msingi ya kuendelea kuishi pekee.
Huduma za afya, mifumo ya maji na usafi wa mazingira, makazi na vyanzo vya riziki bado vimeharibiwa vibaya, na kuwaacha familia katika hatari kubwa hususan wakati wa majira ya baridi imesema ripoti
Usitishaji mapigano wa kudumu wahitajika
“Familia zinavumilia yasiyovumilika,” Bwana Guterres ameeleza hali mbaya ya watoto wanaolala katika mahema yaliyojaa maji na majengo yanayoanguka kutokana na mvua kubwa na upepo mkali.
Amesema timu za kibinadamu zinaandaa zaidi ya milo ya moto milioni 1.5 kila siku, zinafungua tena vituo vya lishe na kurejesha huduma za maji na afya, lakini akaonya kuwa mahitaji yanaendelea kukua kwa kasi kuliko uwezo wa utoaji wa misaada.
“Tunahitaji usitishaji mapigano wa kweli na wa kudumu,” amesema, akitoa wito wa kufunguliwa kwa vivuko zaidi kuingia Gaza, kupunguzwa kwa vikwazo vya bidhaa muhimu, kuwepo kwa njia salama ndani ya Ukanda, ufadhili endelevu na upatikanaji wa misaada ya kibinadamu bila vikwazo.
Ripoti ya IPC inasisitiza kuwa bila upatikanaji endelevu wa misaada na uliopanuliwa, kuendelea kwa misaada, na ujenzi upya wa miundombinu muhimu, hali ya uhakika wa chakula Gaza inaweza kuzorota kwa kasi tena, na kusababisha madhara ya muda mrefu kwa wakazi ambao tayari wameathiriwa kisaikolojia.