
Ukizubaa umeachwa. Ndiyo hali ilivyo katika mbio za kuwania kukaa kileleni mwa Ligi Kuu England ambapo leo michezo nane itafanyika kwenye viwanja tofauti nchini humo.
Mchezo wa mapema utapigwa saa 9:30 Alasiri kwenye Uwanja wa St Jamie’s Park, ambapo Newcastle United itakuwa nyumbani kuikaribisha Chelsea ya Enzo Maresca.
Newcastle itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na rekodi nzuri ya kupata matokeo mazuri dhidi ya Chelsea ikiwa kwenye dimba lake hilo la nyumbani kwani katika mechi tano ilizocheza hapo dhidi ya ‘The Blues’, imepata ushindi mara nne na kupata sare mara moja.
Iwapo Chelsea itaibuka na ushindi katika mchezo huo, itajihakikishia kubakia katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa EPL kwani hadi sasa imekusanya jumla ya pointi 28 mbele ya Crystal Palace ambayo inashika nafasi ya tano ikiwa na pointi 26 na iwapo Chelsea itashindwa kupata matokeo mazuri, Crystal Palace inaweza kuishusha kama itashinda mechi yake dhidi ya Leeds.
Mchezo mwingine ambao utafuatiliwa sana na wapenzi wa soka, utapigwa kwenye Uwanja wa Etihad, saa 12:30 jioni, wakati Manchester City itakuwa nyumbani dhidi ya West Ham United.
Katika mchezo huu, Man City itaingia uwanjani kibabe kwani inashikilia rekodi ya kupata ushindi katika michezo 16 na kupata sare mara tatu katika mechi 19 ilizocheza na West Ham.
Mara ya mwisho kwa West Ham kuifunga Man City ilikuwa ni Oktoba 27, 2021 iliposhinda kwa mikwaju ya penalti katika raundi ya nne ya Kombe la Carabao na kuiondosha City kwenye mashindano hayo.
Kama Man City itaendeleza rekodi yake ya ushindi leo dhidi ya West Ham basi vijana wa Pep Guardiola watakwea hadi kileleni mwa msimamo wa EPL kwa pointi 37 kwani itakuwa na pointi moja mbele dhidi ya Arsenal ambayo ndiyo inaongoza ligi hadi saa kwa pointi 36.
Mchezo mwingine wa kukata na shoka utakuwa kati ya Tottenham dhidi ya Liverpool utakaochezwa majira ya saa 2:30 usiku.
Katika mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Tottenham Hotspurs, utakuwa wa aina yake kwani vijana wa Thomas Frank watakuwa na kibarua cha kuvunja uteja dhidi ya kikosi cha Majogoo wa Anfield ambacho kimekuwa na ubabe kwa muda mrefu.
Msimu uliopita vijana wa Arne Slot walipata matokeo ya ushindi katika mechi zote mbili dhidi ya Spurs huku katika mechi tano za mwisho Liverpool imepata ushindi mara nne na kupoteza mara moja.
Katika mchezo wa leo mshambuliaji wa Liverpool, Alexander Isak ataingia na rekodi ya kuifunga Spurs mabao sita katika mechi nne za mwisho alizocheza dhidi yao wakati kwa upande wa Tottenham, mshambuliaji Richarlison ndiye amehusika kwenye mabao mengi dhidi ya Liverpool akiwa amefunga manne na kutoa pasi tatu za mwisho.
Matokeo ya ushindi yataifanya Liverpool kufufua matumaini ya kuwania zile nafasi nne za juu baada ya mfululizo wa matokeo mabaya katika michezo iliyopita.
Kwa upande wa Spurs, hawajaonesha kiwango kizuri hadi sasa kwani katika michezo 16 iliyocheza imepata ushindi mara sita, sare nne na vipigo sita ikiwa inashika nafasi ya 11 kwa pointi 22.
Mchezo mwingine mkali utazikutanisha Everton dhidi ya vinara wa ligi, Arsenal ambayo itakuwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha inapata matokeo ya ushindi ili kuendelea kuongoza msimamo wa EPL.
Mchezo huo utachezwa kuanzia saa 5:00 usiku kwenye Uwanja wa Hill Dicksons ambao Arsenal itashuka kwa mara ya kwanza tangu Everton kuanza kuutumia uwanja huo msimu huu ikihama kutoka Goodson Park.
Msimu uliopita hakukuwa na mbabe kati ya timu hizi mbili baada ya kutoka sare mechi zote mbili wakati katika jumla ya michezo mitano iliyopita Arsenal imeshinda mara tatu na kutoka sare mara mbili.
Iwapo Arsenal itapata matokeo ya ushindi kwenye mchezo huu, itakuwa ni mara ya tano kuongoza msimamo wa ligi katika kipindi cha sikukuu za Christmas huku ikiwa ni mara ya tatu katika kipindi cha miaka minne ambayo Arsenal imekuwa ikikaa kileleni lakini ikashindwa kuchukua Ubingwa.
Kocha Mikel Arteta anapaswa kujua mwaka 2026 unatakiwa kuwa mwaka wa mafanikio kwa washika mitutu wa London kwani katika mechi ya leo ndiyo ya kumaliza mwaka 2025 na kwamba hatopewa zawadi yoyote kutoka kwa wapinzani wao hao ambao aliwatumikia kwa kipindi cha miaka sita kama mchezaji na vinginevyo atakuwa na kibarua kizito cha kuhakikisha anaondoka na pointi tatu muhimu.
Michezo mingine ya EPL itakayopigwa leo
Brighton vs Sunderland
Wolves vs Brentford
Leeds vs Crystal Palace