
Musoma. Zaidi ya Sh9.8 bilioni zimekopeshwa kwa wafanyabiashara ndogondogo 4,324 nchini kuanzia Machi 2024 hadi sasa, ambapo kati ya fedha hizo Sh428 milioni zimekopeshwa kwa wafanyabiashara 244 mkoani Mara.
Hayo yamesemwa leo Desemba 22, 2025 mjini Musoma na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Maryprisca Mahundi, alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara ndogondogo kuhusu fursa za mikopo ya Serikali.
Amesema mbali na fedha hizo, Serikali imetenga zaidi ya Sh5.5 bilioni zitakazotolewa Novemba mwaka huu kwa ajili ya kuwawezesha wafanyabiashara ndogondogo kuboresha shughuli zao na hatimaye kukua kiuchumi. Fedha hizo tayari zimekabidhiwa Benki ya NMB, ambayo imepewa jukumu la kuzitoa kwa walengwa.
Mahundi ameitaka NMB kuhakikisha mikopo hiyo inawafikia walengwa bila urasimu, akisisitiza Serikali haitavumilia fedha hizo kuwafikia wasiostahili.
“Hatutakubali mikopo hii ifike kwa wasiokuwa walengwa. Kufanya hivyo ni kumuangusha Rais wetu ambaye ameonesha dhamira ya dhati ya kuwainua wafanyabiashara ndogondogo,” amesema.
Amesema wafanyabiashara ndogondogo ni nguzo muhimu ya uchumi wa Taifa kuanzia ngazi ya familia, hivyo Serikali imeamua kuwaweka katika mfumo rasmi ili wapate haki na fursa mbalimbali za kiuchumi.
Ili kunufaika na mikopo hiyo, Mahundi amewataka wafanyabiashara kujisajili katika mfumo wa kidijitali. Amesema tangu kuanza kwa usajili Machi 2024, wafanyabiashara zaidi ya 115,000 wamesajiliwa, wakiwemo wanawake zaidi ya 44,500. Mkoa wa Mara una wafanyabiashara 5,338 waliosajiliwa.
Baadhi ya wafanyabiashara wameipongeza Serikali kwa hatua hiyo wakisema itasaidia kutatua changamoto ya mitaji. Neema Amos amesema ukosefu wa mitaji umekuwa kikwazo kikubwa, huku mikopo kutoka taasisi zisizo rasmi ikiwasababishia wengi kufilisika.
“Hii ni fursa kwetu kutoka biashara ndogo kwenda za kati na hatimaye kubwa,” amesema.
Naye Joyce Manyama ameomba kuondolewa kwa vikwazo na urasimu katika upatikanaji wa mikopo hiyo, akisema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakikumbana na changamoto wakati wa kuomba, ingawa Serikali imeanza kuzifanyia kazi.