Mratibu wa Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa, na mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu misaada ya kibianadamu OCHA Tom Fletcher, ametenga dola milioni 1 kutoka Mfuko wa Dharura wa Umoja wa Mataifa CERF, ili kusaidia hatua za haraka za sekta ya afya dhidi ya mlipuko huo, ambao umekuwa ukienea tangu katikati ya Septemba, kulingana na taarifa iliyotolewa na OCHA.

Fedha hizo zitasaidia utekelezaji wa huduma za kuokoa maisha katika majimbo ya Mopti, Ségou na Tombouctou katikati na kaskazini mwa nchi, ambako viwango vya vifo vimeripotiwa kuwa vya juu zaidi.

Zaidi, ya visa 530 vimeripotiwa

Hadi mwanzoni mwa mwezi huu wa Desemba, mamlaka za afya nchini Mali zilikuwa zimeripoti zaidi ya kesi 530 zilizothibitishwa za donda koo na zaidi ya vifo 30.

Hata hivyo, mashirika ya kibinadamu yanaonya kuwa idadi halisi huenda ikawa kubwa zaidi kutokana na kuripotiwa kwa kiwango kidogo, hasa katika maeneo magumu kufikika na yaliyoathiriwa na migogoro.

Mlipuko huu unatokea wakati Mali ikiendelea kukabiliwa na changamoto sugu, zikiwemo upatikanaji mdogo wa huduma za afya, upungufu wa chanjo za kawaida na ukosefu wa usalama unaoendelea.

Harakati za watu kuvuka mipaka ya nchi pia zimeongeza hatari ya maambukizi, jambo linalozidisha ugumu wa kudhibiti ugonjwa huo.

OCHA imesema kuwa mgao huo kutoka CERF utawezesha Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO kuongeza kasi ya hatua zake, ikiwemo kupeleka timu za dharura za kitabibu, kusambaza dawa za vijiua vijasumu au antibiotiki na dawa za kupunguza sumu ya diphtheria au antitoxins, pamoja na kuimarisha hatua za kuzuia na kudhibiti maambukizi.

Usimamizi wa wagonjwa

Kwa mujibu wa OCHA hatua hizo pia zitauunga mkono usimamizi wa wagonjwa, ufuatiliaji wa waliokutana na wagonjwa na kampeni za uhamasishaji wa jamii ili kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa huo.

CERF, mfuko wa dharura wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa, umeundwa kuhakikisha kuwa msaada wa kibinadamu unawafikia watu walio katika hali ya dharura kwa haraka iwezekanavyo.

Mgao huu wa hivi karibuni unaonesha wasiwasi unaoongezeka ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhusu uwezekano wa mlipuko huu kusambaa zaidi iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

Washirika wa kibinadamu wanasema kuwa uingiliaji wa haraka ni muhimu ili kuzuia vifo zaidi, hususan miongoni mwa watoto, ambao wako katika hatari kubwa zaidi ya kuathiriwa na diphtheria katika mazingira yenye chanjo duni na mifumo ya afya iliyo chini ya shinikizo kubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *