Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) ni miongoni mwa vyama vya wafanyakazi vinavyounganisha wafanyakazi kutoka sekta za viwanda, biashara, taasisi za fedha, huduma na ushauri.
Chama hiki kinafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Wafanyakazi nchini na ni mshirika wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzani (TUCTA) tangu mwaka 1998. TUICO kinafanya kazi na kutekeleza majukumu yake kupitia muundo thabiti unaowezesha na kuhakikisha uwakilishi mzuri wa wanachama katika ngazi zote.
Msingi wa Chama unaanzia katika ngazi ya tawi, ambalo linaundwa na wanachama wote wa TUICO katika mahali pa kazi. Kila tawi linaongozwa na Mwenyekiti, Katibu, na Halmashauri ya Tawi, huku ukubwa wa uongozi ukiwa unategemea idadi ya wanachama katika tawi husika.
Matawi yote hulelewa na ofisi za mikoa, TUICO ina ofisi 22 za mikoa pamoja na ofisi nne ndogo, kila moja ikiwa na ofisi chini ya uongozi wa katibu wa mkoa. Ofisi hizi za mkoa huratibu shughuli za chama matawini, kusaidia matawi pia kusimamia utekelezaji wa mipango mbalimbali ya chama katika mikoa husika.
Ofisi za kanda hukusanya mikoa kadhaa iliyo karibu kijiografia. TUICO ina ofisi nane za kanda kote nchini, kila moja ikiwa chini ya uongozi wa Katibu wa Kanda. Ofisi za kanda zinashirikiana na kusimamia uhusiano kati ya ngazi ya mkoa na uongozi wa kitaifa.
Ngazi ya juu zaidi ya utekelezaji majukumu ya chama, ni ngazi ya Taifa. Ambayo huratibu shughuli zote za chama kwa ngazi ya Taifa chini ya usimamizi wa Katibu Mkuu.
Ili kurahisisha utendaji na uratibu TUICO ina sekta nne kuu zinazowakilisha maeneo tofauti ya kazi; viwanda, biashara, taasisi za kifedha, na huduma na ushauri. ambazo zinasaidiwa na idara nne ambazo ni fedha na utawala, elimu na vijana, sheria na wanawake, afya na usalama. pamoja na vitengo vitatu, uhamasishaji na uhusiano wa kimataifa, ukaguzi wa ndani, na uchumi, takwimu na teknolojia ya habari na mawasiliano.
Muundo huu wa kiutendaji unakazi kuu ya kusimamia na kutekeleza shughuli kuu za chama ambazo ni;
Uandikishaji na ukusanyaji wa wanachama
Chama kinapanga shughuli za kuandikisha na kukusanya wanachama wapya ili kuimarisha uwakilishi wa pamoja. Kupitia ziara za moja kwa moja katika sehemu za kazi, wafanyakazi wanahamiasishwa kujiunga, kushiriki, na kuchangia katika maamuzi yanayowagusa.
Wanachama wa TUICO wakiwa kwenye moja ya mikutano ya chama hicho yenye lengo la kudumisha mawasiliano na wanachama.
Mikataba ya Kazi ya Pamoja (CBAs)
Jukumu lingine kuu la Chama ni kufunga na kushiriki majadiliano ya Mikataba ya Hali Bora (CBA). Hili linapelekea kuboresha mazingira ya kufanyika kazi yawe katika hali ya kiusalama na afya jambo ambalo litakuwa kivutio na kuwatia moyo wafanyakazi waendelee kutekeleza wajibu wao kwa ukamilifu.
Utoaji wa elimu na mafunzo
Chama kimeendelea kuandaa programu za mafunzo kwa lengo la kuimarisha elimu na ufahamu wa wafanyakazi. Mafunzo haya yanahusisha haki za wafanyakazi, uongozi, mazungumzo, usalama kazini na usimamizi wa chama, na kuruhusu wanachama kujitetea na kuwakilisha wengine kwa ufanisi.
Utatuzi wa migogoro
Chama kimeendelea kusimamia na kusaidia wafanyakazi kushughulikia migogoro pale inapotokea. Hii inajumuisha kutoa ushauri, kushirikiana na uongozi, na kufuata njia za suluhisho za haki kupitia mazungumzo au taratibu rasmi inapohitajika.
Uundaji na kamati mbalimbali
Chama kinaanzisha na kuunda kamati mbalimbali pia kutoa elimu juu ya kamati hizo, hili ni kupitia kushirikiana na waajiri katika kuhakikisha makundi maalumu (wanawake, vijana na watu wenye ulemavu) yanapata haki sawa na wafanyakazi wengine mahali pa kazi. Miongoni mwakamati hizo ni Kamati za Wanawake, Vijana, Usalama na Afya Kazini (OHS).
Mikutano ya wafanyakazi na ziara za mahali pa kazi
Chama kimeendelea kufanya mikutano ya mara kwa mara na ziara za mahali pa kazi hufanyika ili kudumisha mawasiliano na wanachama. Fursa hii inatoa njia za kutambuana, kukusanya maoni, na kujadili changamoto kazini moja kwa moja na wafanyakazi.
Uchapishaji wa jarida
Chama kinatengeneza na kusambaza jarida (Sauti ya TUICO) kwa lengo la kuwajulisha wanachama kuhusu shughuli, maendeleo ya sera, mafanikio, na masuala yanayojitokeza. Hii husaidia kukuza uwazi, uelewa, na ushirikiano wa kudumu miongoni mwa wanachama.
Wanachama wa TUICO wakiendelea na programu ya mafunzo kwa lengo la kuimarisha elimu na ufahamu wa wafanyakazi.
Kupitia utekelezaji huu wa shughuli za chama, TUICO imeendelea kujihakikishia kuwa wanachama na wafanyakazi wanafikiwa na uandikishaji na uhamasishaji, Wananufaika na Mikataba ya Hali bora, Wanapata elimu na mafunzo, malalamiko na migogoro inashughulikiwa, na wanapata taarifa kuhusu chama kwa wakati sahihi. Hivyo tumeendelea kupata matokeo chanya katika kuboresha hali za kazi, kuimarisha uwakilishi na kuongeza uelewa miongoni mwa wanachama.
Kwa zaidi ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, TUICO imeendelea kuwa nguzo muhimu ya kutetea maslahi ya wafanyakazi nchini Tanzania, kupitia utekelezaji wa majukumu yake ya uwakilishi, mafunzo, mashauriano ya pamoja, na kuendeleza demokrasia ndani ya chama. Mafanikio mengi yanayoonekana leo ni matokeo ya kazi imara iliyotekelezwa na viongozi na wanachama wa chama kwa miongo kadhaa.