
Harakati za vyama vya wafanyakazi Tanzania zimepitia katika vipindi tofauti vya kisiasa na kiuchumi. Harakati hizo ziliendeshwa wakati wa ukoloni na baada ya uhuru. Kabla ya uhuru (Wakati wa Ukoloni) vyama vya wafanyakazi viliendeshwa kwa uhuru na usawa lakini baada ya uhuru vilikuwa sehemu ya chama tawala.
Kwa mfano, kati ya mwaka 1964 na 1978 NUTA ilikuwa ni sehemu ya Tanganyika African National Union (TANU). Pia kati ya miaka ya 1978 hadi 1991 Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania (JUWATA) ilikuwa ni moja ya Jumuiya muhimu ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Tofauti hizi hazikuathiri tu miundo ya vyama vya wafanyakazi lakini pia zilichangia kubadili tabia na mitizamo yake.
Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) ni chama cha pekee cha wafanyakazi hapa Tanzania kinachohudumia wafanyakazi kutoka taasisi za umma na binafsi na kinaundwa na sekta nne ambazo ni viwanda, biashara, taasisi za fedha, huduma na ushauri.
Vyama vya wafanyakazi vimekuwa vikisukumwa na matukio mbalimbali yanayotokana na mabadiliko katika mifumo ya kijamii na kiuchumi, aidha mabadiliko ya kiuchumi yaliyoikumba nchi miaka ya 90 pia yalibadili mfumo wa Vyama vya Wafanyakazi.
TUICO kilianzishwa mwaka 1995 pamoja na vyama vingine 10 na kujishirikisha katika Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania Federation of Free Trade Union (TFTU) mwaka 1998 na baadae TUCTA (Trade Union Congress of Tanzania) mwaka 2001.
Kwa takribani miongo mitatu, TUICO si tu kimekuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za wafanyakazi, bali pia kimekuwa kiunganishi cha mahitaji ya uchumi unaobadilika na kulinda heshima na ustawi wa wafanyakazi.
Kama inavyofahamika kuwa, uchumi wa Tanzania umepitia mabadiliko makubwa tangu miaka ya 1990 ubinafsishaji, uwekezaji wa kigeni, uanuwai wa viwanda na kuibuka kwa huduma za kidijitali. Ingawa haya yameongeza ajira, pia yameleta changamoto, usalama wa ajira umepungua, mikataba ya muda mfupi imeenea, na wafanyakazi wengi wamejikuta wakifanya kazi katika mazingira yasiyo rasmi au yenye maslahi duni.
Katika muktadha huu wa mabadiliko, TUICO imeendelea kuwa thabiti katika kukabiliana na changamoto hizo. Kupitia majadiliano ya pamoja na mikataba ya hali bora (CBAs) ili kuboresha mishahara, kuhakikisha haki, na kuimarisha ulinzi wa maslahi kwa maelfu ya wafanyakazi. Mikataba hii iliyopkina na waajiri imeleta mabadiliko chanya katika maisha ya wafanyakazi wengi nchini.
Kwa TUICO, harakati hizi si suala la mishahara pekee ni jitihada za kulinda na kuboresha utu na hadhi ya mfanyakazi katika dunia ya ajira. Tukiwa na mtazamo kuwa wafanyakazi si mshirika muhimu wa maendeleo ya Tanzania, bali ni injini ya maendeleo inayostahili usalama, maisha ya heshima, na sauti katika kuamua mustakabali wao.
Ustawi na usawa wa kijinsia
Mbali na kulinda masilahi ya wafanyakazi, juhudi za chama hazijaishia kwenye majadiliano ya mishahara pekee. Kimeendelea kusimamia pia ajenda ya kujenga mazingira ya kazi yenye haki ikizingatia ustawi na usawa wa kijinsia kwa mapana yake, kupitia kushinikiza upatikanaji wa bima ya afya kwa wafanyakazi na wategemezi wao, posho za makazi, posho za usafiri na mafao ya pensheni chini ya mfumo wa hifadhi ya jamii wa Tanzania.
Katika mapambano yetu ya kila siku, tumejitolea kuendeleza usawa wa kijinsia katika sehemu za kazi. Katika sekta kama benki, huduma za wageni, na biashara za rejareja ambazo zina wafanyakazi wengi wanawake, tumeendelea kusimamia malipo sawa kwa kazi sawa, ulinzi dhidi ya unyanyasaji kazini na kuhakikisha wanawake wanawakilishwa ipasavyo katika nafasi za uongozi, si tu katika maeneo ya kazi bali pia ndani ya chama chetu.
Pia kupitia programu zetu za kujenga uwezo, tumewawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika majadiliano na mchakato wa kufanya maamuzi. Kwa njia hii, tunapambana na tofauti za kijinsia ambazo bado zinaathiri sekta nyingi, na tunajenga mazingira ya haki na usawa kwa kila mfanyakazi.
Kipaumbele kwa usalama kazini
TUICO imejizatiti kuvisimamia ni kuhakikisha usalama na afya mahali pa kazi. Kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) na wadau wengine, tumekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanapewa mafunzo, vifaa na uelewa wa kutosha ili kudai mazingira salama ya kazi.
Katika viwanda, maghala, na biashara mbalimbali, tumeendelea kutetea utekelezwaji wa sheria za usalama za kitaifa, kuhimiza ukaguzi wa mara kwa mara wa sehemu za kazi, na kushinikiza upatikanaji wa vifaa kinga kwa wafanyakazi. Juhudi zetu zisizochoka zimechangia kupungua kwa ajali na vifo kazini, na hivyo kuthibitisha kuwa kulinda maisha ya wafanyakazi si jambo linalowezekana tu, bali ni la lazima.
Pamoja na hayo, tunashirikiana kwa karibu na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ili kuhakikisha kuwa wale wanaoumia au kuathirika kiafya kutokana na kazi zao wanapata fidia stahiki kwa wakati muafaka