MABINGWA mara moja wa Kombe la Mapinduzi mwaka 2016, URA wameanika mikakati yao katika mashindano hayo yaliyoanza Desemba 28, 2025 yakichezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.

URA kutoka Uganda ambayo jana saa 10:15 jioni ilikuwa uwanjani kucheza dhidi ya Mlandege, ilikuwa ni mechi yao ya kwanza kundi A baada ya ile dhidi ya Azam iliyopangwa kuchezwa Desemba 28, 2025 kusogezwa mbele hadi Januari 5, 2026 kutokana na changamoto ya usafiri waliyokutana nayo iliyowafanya kuchelewa kituo cha mashindano.

Kocha Msaidizi wa URA, Ssemuyaba Bashir, amesema wanayatumia mashindano hayo kama fursa ya kujiimarisha zaidi kabla ya kurejea katika Ligi ya Uganda kuendelea na mchakamchaka wa msimu huu wa 2025-2026.

Mbali na hilo, amesema wanatumia kutoa fursa kwa wachezaji wao wanaochipukia kujiimarisha zaidi.

“Sisi URA sio timu ngeni visiwani Zanzibar kwani tuliwahi kuwa hapa na kubeba ubingwa (2016) lakini safari hii tumekuja n kukuta mazingira tofauti kabisa ikiwamo uwanja.

“Tupo hapa kwa ajili ya mashindano, malengo yetu ni kuona tunashinda ubingwa, tuna wachezaji wazoefu na wanaochipukia, hivyo tumekuja nao kuwapa uzoefu.

“Naweza kusema Kombe la Mapinduzi ni fursa kwa timu zote za Afrika Mashariki tukiwemo sisi kwa sababu huzikutanisha timu mbalimbali za ukanda huu,” amesema Bashir.

URA iliyopo kundi A, baada ya kucheza dhidi ya Mlandege, ratiba inaonyesha Januari 3, 2026 itakabiliana na Singida Black Stars, kisha Januari 5, 2026 itamaliza hatua ya makundi dhidi ya Azam. Timu hiyo katika Ligi Kuu ya Uganda msimu huu 2025-2026, inashika nafasi ya 10 ikiwa na pointi 11 baada ya kucheza mechi 11. Imeachwa pointi 15 na kinara KCCA.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *